Carlinho kawa mtamu balaa

Wednesday April 07 2021
carinopic
By Thomas Ng'itu

WINGA wa Yanga, Carlos Fernandes 'Carlinho' amezidi kuimarika kimwili na kisaikolojia kadri siku zinavyozidi kusonga mbele hivyo mabeki wa timu pinzani kwenye Ligi Kuu Bara wanatakiwa kujipanga.
Mwanaspoti ambalo jana Jumanne April 6 lilikuwa katika uwanja wa Avic Town, lilimshuhudia mchezaji huyo akipambana katika mchezo wa kirafiki dhidi ya African Lyon ambao Yanga ilishinda  mabao 3-0.
Katika mchezo huo Carlinho alipewa dakika 45 za kipindi cha pili na alipoingia alipambana kuhakikisha analishawishi benchi la ufundi kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza.
Carlinho alikuwa akipambana huku akiwa hawakwepi wapinzani wake bali alikuwa anawafuata na kuwatoka kwa kuwapiga chenga zilizowafurahisha mashabiki wa Yanga waliokuwa wakiangalia mchezo huo .
Mchezaji huyo pia alipokuwa anakutana na ugumu, alikuwa anapambana nao hata kama wakiwa wanavutana miguu alikuwa hakubali kirahisi kuachia mpira.
Awali Carlinho alikuwa ni mchezaji anayecheza kwa uoga, lakini kadri siku zinavyosonga mbele amezidi kuwa fiti katika upande wa fiziki.


Advertisement