Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chelsea ilivyogeuka shamba la bibi kwa makocha

London,England. Imezoeleka kuona timu zikitumia kiasi kikubwa cha fedha katika mchakato wa usajili wa wachezaji kutoka timu nyingine iwe kwa kuvunja mikataba au kunyakua wale walio huru.

Fedha hizo ama hutumika kulipa ada za usajili ambazo klabu huhitaji ili kuwaachia wachezaji wao wenye mikataba au kuingiza katika akaunti binafsi za wale waliomaliza mikataba lakini pia mishahara kwao mara baada ya kujiunga nazo.

Lakini katika miaka mingi ya hivi karibuni, mambo yanaonekana kuwa tofauti na makocha wamekuwa wakizigharimu klabu fedha nyingi katika kuvunja mikataba yao na wengine kwa mishahara wanayolipwa katika timu wanazojiunga nazo.

Uhamisho uliofanywa hivi karibuni na Chelsea wa kumchukua Enzo Maresca umeifanya iendelee kuwa miongoni mwa klabu chache katika miaka ya hivi karibuni ambazo zimetumia kiasi kikubwa cha fedha katika kuajiri, kuishi na hata pale zinapotimua makocha.

Baada ya kuachana na Mauricio Pochettino kwa makubaliano binafsi mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2023/2024, Chelsea iliamua kumnyakua kocha aliyeiongoza Leicester City kutwaa ubingwa wa Ligi ya Championship msimu uliomalizika na kuiongoza kurudi Ligi Kuu England (EPL), Enzo Maresca.

Maresca (44), alikuwa ametumikia mkataba wake na Leicester City, mwaka mmoja tu kati ya mitatu ambayo alisaini wakati anajiunga nayo mwaka jana hivyo Chelsea imelazimika kutoa kitita cha Pauni 10 milioni ili kuvunja mkataba wa kocha huyo na kumpa kazi ya kunoa kikosi chao.

Kocha huyo alionekana ana sifa nyingi ambazo ziliivutia Chelsea na kuamua kumpa ajira akiwapiku makocha wengine watatu ambao walikuwa miongoni mwa iliovutiwa nao ambao ni  Meneja wa Ipswich Town, Kieran McKenna, meneja wa zamani wa Brighton, Roberto De Zerbi na meneja wa Brentford, Thomas Frank.

Kwa kiasi hicho cha fedha ambacho Chelsea imelipa ili kupata huduma ya Maresca, meneja huyo anaingia katika nafasi ya tano katika chati ya makocha ambao klabu wanazofundisha au walizowahi kufundisha zilitoa kiasi kikubwa cha fedha za kuvunja mikataba kwenye klabu zao za zamani ili kuwavuta kunoa vikosi vyao.

Orodha hiyo inaongozwa na Julian Nagelsmann ambaye mwaka 2021, Bayern Munich ilitumia kiasi cha Pauni 21.7 milioni kuvunja mkataba wake na RB Leipzig lakini alidumu kwa miaka miwili tu akiiongoza miamba hiyo ya Ujerumani katika mechi 84 tu kisha kuachana nayo na kujiunga na timu ya taifa ya nchi hiyo.

Anayefuatia ni Graham Potter ambaye alikuwa ni kocha wa pili kuchukuliwa na Chelsea tangu ilipoanza kuwa chini ya utawala wa bilionea, Todd Boehly, uhamisho uliofanyika mwaka 2022.

Wakati Chelsea inafikia uamuzi wa kumchukua Potter, alikuwa na mkataba na Brighton hivyo bilionea Boehly alilazimika kulipa kiasi cha Pauni 21.5 milioni kwa Brighto ili imruhusu kocha huyo kuondoka.

Mwaka 2011, Chelsea ilimchukua Andre Villa Boas aliyekuwa kocha wa Porto na uhamisho huo uliigharimu kiasi cha Pauni 13.2 milioni na kumfanya awe kocha wa tatu ambaye mkataba wake ulivunjwa kwa kiasi kiikubwa cha fedha.

Uhamisho uliofanywa na Bayern Munich hivi karibuni wa kumchukua aliyekuwa kocha wa Burnley, Vincent Company kwa Pauni 10.22 milioni unashika nafasi ya nne nyuma ya Andre Villa Boas na nafasi ya tano ndio yupo Maresca.

Katika nafasi ya sita, uhamisho ghali kwa makocha ni wa hivi karibuni ambao Liverpool wameufanya kwa kumchukua kocha wa Feyenoord, Arne Slot wa Pauni 9.42 milioni na nafasi ya saba ni uhamisho wa Brendan Rodgers kutoka Celtic kwenda Leicester City mwaka 2019 ambao uligharimu kiasi cha Pauni 8.8 milioni.

2019, Sporting ilimnyakua Ruben Amorim kutoka Braga kwa Pauni 8.4 milioni, uhamisho ambao unashika nafasi ya nane kwa kuwa ghali upande wa makocha, nafasi ya tisa inashikwa na uhamisho wa Jose Mourinho wa kutoka Inter Milan kwenda Real Madrid mwaka 2010 ambao ulikuwa wa Pauni 6.9 milioni na unaoshika nafasi ya 10 ni wa Mourinho tena pindi alipojiunga na Chelsea mwaka 2004 kutoka Porto ambao ulikuwa wa Pauni 5.2 milioni.

Kwa mantiki hiyo, katika orodha ya makocha 10 ambao uhamisho wao ni ghali zaidi duniani, wanne ni waliojiunga na Chelsea kwa nyakati tofauti.

Katika kudhihirisha namna Chelsea ilivyo haigopi kutumia fedha ili kupata kocha inayemhitaji, kuanzia mwaka 2000 hadi sasa, imetumia kiasi cha Pauni 55.5 milioni katika kunyakua makocha.