Vita ya Haaland, Keane yazidi kupamba moto

Nyota wa Manchester City, Erling Haaland na mchambuzi wa soka, Roy Keane wanakaribia kufikia pabaya kutokana na mrushiano wa maneno unaoendelea baina yao tangu mchambuzi huyo alipotoa maneno yaliyoonekana kama kejeli kwa Halaand mwezi Machi wakati Manchester City ilipotoka sare nyumbani na Arsenal.

Keane alimfananisha Haaland na mchezaji wa Ligi Daraja la tatu akidai alionyesha kiwango kibovu katika mchezo huo uliomalizika kwa matokeo ya kufungana bao 1-1.

Hata hivyo baada ya kuiongoza Manchester City kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Wolves, mwishoni mwa wiki iliyopita, Haaland amejibu mapigo kwa Keane akisema kuwa hajali wala kufuatilia kile kinachosemwa na kiungo huyo wa zamani wa Manchester United.

"Sijali kabisa kuhusu huyo mtu hivyo kila kitu ni sawa. Sijali, tunatakiwa kushinda mechi zetu," alisema Haaland.

Katika mchezo dhidi ya Wolves, Haaland alifumania nyavu mara nne yaliyomfanya azidi kujikita kileleni katika chati ya nyota wanaoongoza kwa kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) msimu huu.

Mara baada ya Haaland kumtumia kejeli hizo, Keane naye hakusita kumshambulia tena mshambuliaji huyo wa Norway kwa kumfananisha na soseji ya nyama ya nguruwe iliyochacha.

"Tumemuona Haaland akifanyiwa mabadiliko na kutolewa nje. Hakuonekana na furaha na alionyesha tabia za 'brat' (soseji ya nyama ya nguruwe) iliyochacha," alisema Keane.