Dabo: Wala hatushindani na Yanga
Muktasari:
- Matajiri hao walipunguza pengo dhidi ya Yanga baada ya ushindi wa 1-0 mbele ya Singida FG kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, kumaliza ukame wa pointi tatu waliokuwa wameukosa kwenye mechi mbili za nyuma walipoambulia sare mfululizo kwa Prisons na Tabora United.
Mwanza. KOCHA Msaidizi wa Azam, Yousuph Dabo amesema hawezi kujiweka kwenye ushindani dhidi ya Yanga katika mbio za ubingwa Ligi Kuu bali kipaumbele chao ni kushinda mechi zao ili kufikia malengo, huku akimbebesha zigo Ayoub Lyanga.
Azam FC ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 40, huku Yanga ikiwa kileleni na alama 43 ikiwa na mechi mbili mkononi, wakati Simba iking’ang’ania nafasi ya tatu kwa alama 36 na faida ya michezo mitatu mkononi.
Matajiri hao walipunguza pengo dhidi ya Yanga baada ya ushindi wa 1-0 mbele ya Singida FG kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, kumaliza ukame wa pointi tatu waliokuwa wameukosa kwenye mechi mbili za nyuma walipoambulia sare mfululizo kwa Prisons na Tabora United.
Dabo alisema ushindi walioupata umeongeza kujiamini na kupunguza presha lakini wanahitaji kubaki kwenye malengo yao kwa kuhakikisha wanacheza mechi kwa ufanisi bila kufikiria wapinzani.
"Hatuwezi kuangalia wapinzani wanafanya nini, tukijikita kuwaangalia wao tutapoteza malengo yetu, hivyo ili kutotoka msitari wetu ni kushinda kila mchezo wetu,” alisema Dabo.
Kuhusu kuwakosa mastaa wake akiwamo Prince Dube, Allassane Diao na Franklin Navaro, Kocha huyo alisema licha ya kuwapo pengo lao, lakini Azam ina wachezaji wengi wenye kuziba nafasi hizo.
“Mechi ya tatu hii tunacheza bila mshambuliaji silaumu lakini napambana kupata tiba ya hili tatizo kwa kuwapa nafasi wachezaji wengine, akiwamo Ayoub Lyanga” alisema.