Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

De Bruyne, Alvarez waipasua Man City

Muktasari:

  • Mkataba wa De Bruyne umebakiza mwaka mmoja kumalizika na bado mazungumzo ya kuongeza mpya hayajaanza wakati Julian Alvarez amekuwa akisisitiza kuwa anahitaji kupata nafasi ya kutosha ya kucheza.

Orlando, Marekani. Licha ya kuamini kuwa Kevin De Bruyne na Julian Alvarez watabakia klabuni, kocha wa Manchester City Pep Guardiola ameonyesha wasiwasi kuwa wanaweza kufanya uamuzi mgumu wa kuachana na timu yake katika dirisha la usajili linaloendelea.

Mkataba wa De Bruyne umebakiza mwaka mmoja kumalizika na bado mazungumzo ya kuongeza mpya hayajaanza wakati Julian Alvarez amekuwa akisisitiza kuwa anahitaji kupata nafasi ya kutosha ya kucheza.

De Bruyne amekuwa akihitajika kwa udi na uvumba na klabu za Saudi Arabia hasa Al Ittihad na ziko tayari kumpa ofa nono ili akubali kujiunga na mojawapo kati ya hizo na hadi sasa nahodha huyo wa Ubelgiji hajatoa muelekeo juu ya hatima yake.

Guardiola alisema kuwa bado De Bruyne ni mchezaji muhimu katika kikosi chake hivyo hafikirii kama atamuachia kirahisi.

“Klabu imeniambia haijapokea ofa yoyote kuhusu De Bruyne. Sijui nini kitatokea lakini ninataka abakie.

“Alikuwa hapa kabla sijawasili. Ni mkubwa zaidi (ameitumikia kwa muda mrefu) hapa. Ilitokea kwa David (Silva) kwa mfano na wachezaji wengine. Anayo sifa ya kuamua hatima yake yeye mwenyewe.

“Kile alichokifanya kwetu ni kikubwa hivyo anaweza kuamua. Taarifa niliyonayo sasa ni kwamba atabakia,” alisema Guardiola.

De Bruyne amekuwa mchezaji muhimu wa Manchester City tangu alipojiunga na timu hiyo mwaka 2015 akitokea Wolfsburg kutokana na mchango wake wa mabao na pasi za mwisho ambao amekuwa akipiga.

Katika mechi 382 ambazo Kevin De Bruyne ameichezea Man City kwa miaka tisa, ametoa mchango wa mabao 272, akifumania nyavu mara 102 na pia akipiga pasi za mwisho 170.

Wakati akizungumzia suala la De Bruyne, Guardiola amesema pia hatima ya mshambuliaji Julian Alvarez bado haijulikani na watafanya mazungumzo naye pindi atakapomaliza majukumu ya timu yake ya taifa.

Kwa sasa Alvarez yupo Ufaransa akiitumikia timu ya taifa ya vijana ya Argentina chini ya umri wa miaka 23 inayoshiriki mashindano ya Olimpiki.

Mchezaji huyo amekuwa akishinikiza kupata nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha Man City na ikishindikana ametishia kuwa ataamua kuondoka.

Guardiola amesema kuwa anatambua na kukubali kuwa mchezaji huyo ana haki ya kushinikiza kupata muda wa kucheza lakini hilo litazungumzwa kwa kikao rasmi baina ya klabu na mchezaji huyo pale atakapomaliza kucheza Olimpiki.

“Sifikirii kumtafutia mbadala. Pale atakapomaliza kufikiria, wakala wake atampigia Txiki (Begiristain) na tutaangalia nini kitatokea,” alisema Guardiola.

Guardiola alisema kuwa ndani ya timu yake kuna wachezaji 18 au 19 ambao kila mmoja anatamani kucheza.