De Gea: Hee imekuwaje tena!

Manchester, England. Maswali yamekuwa mengi juu ya wapi anaweza kucheza baada ya kukaa nje kwa zaidi ya nusu msimu, lakini sasa taarifa kutoka The Sun zimefichua kwamba kipa wa zamani wa Manchester United, David de Gea amekataa ofa kubwa ya Pauni 500,000 kwa wiki kwenda kuungana na Cristiano Ronaldo na badala yake anafikiria kuungana na Lionel Messi.
De Gea mwenye umri wa miaka 33, alipewa nafasi ya kuungana na Ronaldo kwenye kikosi cha Al Nassr ya Saudi Arabia katika dirisha lililopita kwa mshahara huo mnono lakini yeye amekataa na kuonyesha nia ya kutua Inter Miami ambako anacheza Lionel Messi.
Kipa huyu raia wa Hispania ambaye kwa sasa yupo huru tangu aachane na Man United katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi baada ya mkataba wake kumalizika alikuwa mmoja kati ya majina makubwa ambayo Al Nassr ilitaka kuyaingiza kwenye timu kama sehemu ya maboresho kwenye kikosi chao.
Kuikataa ofa hii huenda kukazua maswali kwa mashabiki wengi kwamba huenda De Gea anamkubali Messi kuliko Ronaldo ndio maana yupo tayari kutua Marekani kwa pesa kidogo kuliko Saudia kwa pesa nyingi.
Hata hivyo, De Gea alishindwa kukamilisha uhamisho huo kwa mujibu wa The Sun kwa sababu mkewe Edurne hapendi mazingira ya Saudia.
Kwa sasa taarifa zinadai Man United itampa ofa ya mkataba wa muda mfupi baada ya Valencia iliyodaiwa kuwa huenda ikamsajili kuwa na hali mbaya ya kiuchumi.
Hali ya maisha ya Marekani inadaiwa kumpendeza na kumvutia zaidi mke wa De Gea na inaelezwa kuwa Miami imeonyesha nia ya kutaka kumsajili lakini hawataweza kumlipa mshahara mnono kama ule ambao Al Nassr walitaka kumpa.
Mbali ya Messi, Miami pia inawamiliki Jordi Alba na Sergio Busquets waliowahi kuwa karibu na De Gea wakati walipokuwa wakikichezea kikosi cha timu ya taifa ya Hispania.
Kuelekea mwanzoni mwa mwaka ujao, Man United huenda ikakumbana na changamoto ya kutokuwa na kipa wao namba moja Andre Onana ambaye atakuwa kwenye majukumu ya kuitumikia Cameroon kwenye ya AFCON.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Januari 13 hadi Februari 11, ikitegemea hadi hatua gani Cameroon itafikia kwenye michuano hiyo.
Mbadala wa Onana kwa sasa ni Altay Bayindir aliyesajiliwa katika dirisha lililopita akitokea Fenerbahce kwa Pauni 4.3 milioni pia yupo.
Kwa sababu hii De Gea naye anaweza kusajiliwa kwa mkataba wa muda mfupi kutokana na uzoefu wake na uwezekano wa kusajiliwa kwake unaonekana kuwa mkubwa baada ya hivi karibuni kuonekana akiwa matembezini na mastaa mbalimbali wa United ikiwa pamoja na Sergio Reguilon na Bruno Fernandes.