DR Congo yavunja mwiko wa miaka 52 Kombe la Dunia, Italia bado nuksi
Muktasari:
- Mara ya mwisho DR Congo ilishiriki fainali za Kombe la Dunia la mwaka 1974 zilizofanyika Ujerumani.
Guadalajara, Mexico. Bao pekee alilofunga Axel Tuanzebe katika mchezo wa mchujo dhidi ya timu ya Taifa ya Jamaica limetosha kuirudisha DR Congo katika michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Juni mwaka huu Marekani, Canada na Mexico.
Imepita miaka 52 tangu mara ya mwisho DR Congo iliposhiriki michuano hiyo mwaka 1974 wakati huo ikijulikana kama Zaire. Katika michuano hiyo iliyokuwa ikifanyika Ujerumani, DR Congo ilitolewa katika hatua ya makundi huku ikikumbana na kipigo cha fedheha cha mabao 9-0 dhidi ya Yugoslavia.
Katika mchezo wa mchujo uliopigwa usiku wa kuamkia leo huko Guadalajara, Mexico ilishuhudiwa DR Congo wakikata tiketi ya pili kucheza fainali za Kombe la Dunia katika muda wa ziada baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.
Vijana wa kocha, Sebastian Desabre walionesha hali ya kujituma muda wote wakishambulia na kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao hao kutokea Marekani Kaskazini.
Nyota wa DR Congo, Axel Tuanzebe wakati akishangilia baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Jamaica katika mechi ya mchujo ya kufuzu Kombe la Dunia. Picha na Mtandao
Hata hivyo, katika dakika ya 100 ya mchezo Tuanzebe aliihakikishia DR Congo tiketi ya kucheza Kombe la Dunia la mwaka huu baada ya kufunga bao pekee kwa kichwa kilichojaa moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa wa Jamaica, Andre Blake akiwa hana cha kufanya.
Jamaica ambao walikuwa na nyota kama Leon Bailey anayekipiga Ligi Kuu England katika Klabu ya Aston Villa wameshindwa kufuzu kwenye michuano hiyo kwa miaka 28 tangu mara ya mwisho waliposhiriki Kombe la Dunia lililofanyika Ufaransa.
Baada ya kufuzu, DR Congo inaingia katika kundi K lenye timu za Ureno inayoongozwa na nahodha wake, Cristiano Ronaldo, Colombia pamoja na Uzbekistan.
Axel Tuanzebe wakati akifunga bao la ushinbdi kwa upande wa DR Congo katika mechi ya mchujo ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Jamaica. Picha na Mtandao
Kwenye fainali hizo ambazo zimebakiza siku 71 kufanyika kuanzia sasa, DR Congo watakabiliana na Ureno, Juni 17 mwaka huu katika mchezo wao wa kwanza wa kundi K utakaopigwa kwenye Uwanja wa NRG, Texas, Marekani.
Timu nyingine zilizopenya katika michezo ya mchujo iliyopigwa jana ni Sweden ambayo iliitupa nje, Poland kwa mabao 3-2, Italia imetupwa nje kwa mikwaju ya penalti 4-1 na Bosnia & Herzegovina.
Uturuki imefuzu baada ya kuichapa Kosovo bao 1-0 wakati Denmark ikiondolewa na Jamuhuri ya Czech kwa mikwaju ya penalti 3-1.