Dube akabidhiwa viatu vya Mayele
Muktasari:
- Mashabiki na wapenzi wa Klabu ya Yanga macho yao kwa sasa yapo kwa mshambuliaji, Prince Dube ambaye wanategemea kuja kufuta kivuli cha Mayele baada ya mastaa kama Guede na Konikon kushindwa kuonyesha kile walichotarajia.
Dar es Salaam. Ni zamu ya Prince Dube ndani ya Yanga. Hivyo ndivyo unaweza kusema baada ya mfupa walioushindwa Kennedy Musonda, Hafiz Konkoni na Joseph Guede katika kuvaa viatu vya Fiston Mayele ambaye alitimka kikosini hapo msimu wa 2022-2023 ulipomalizika akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara.
Mayele ambaye kwa sasa anakipiga Pyramids FC ya Misri, amehudumu kwa misimu miwili ndani ya kikosi cha Yanga na kufanikiwa kuwa kinara wa mabao kwenye timu hiyo kwa misimu yote hiyo.
Msimu wake wa kwanza ndani ya ligi (2021/22) alifunga mabao 16 akiwa nyuma kwa bao moja dhidi ya aliyekuwa kinara, George Mpole ambaye alifunga mabao 17 akiitumikia Geita Gold.
2022/23 ndio ulikuwa msimu wake wa pili na wa mwisho ndani ya kikosi cha Yanga kabla kutimkia Pyramids FC, aliondoka akiwa ametupia mabao 17 akifungana na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Saidi Ntibazonkiza 'Saido' wakiibuka wafungaji bora.
Baada ya kuacha rekodi hiyo, Mayele alitimka nchini akiwa ametwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) sambamba na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023, kisha akaiacha Yanga ikisafa kusaka mbadala sahihi wa kuziba nafasi yake.
Mayele ndani ya kikosi cha Yanga alicheza kwa kiwango cha juu katika misimu miwili akifunga mabao 33 kwenye Ligi Kuu Bara pekee, nje na michuano mingine ikiwemo ile ya kimataifa ambapo msimu wa 2022-2023 walipocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, alimaliza na mabao saba akiwa kinara.
Hapa kuna takwimu za washambuliaji ambao walitegemewa kuwa ni warithi wa Mayele katika kuzifumania nyavu ndani ya kikosi hicho baada ya staa huyo kuondoka lakini imekuwa tofauti huku kila kipindi cha usajili wakitafutwa washambuliaji wengine katika namna ya kuona dawa inapatikana.
Ikumbukwe kwamba kipindi hiki cha usajili wa dirisha kubwa, Yanga imemsajili mshambuliaji Prince Dube aliyekuwa akiitumikia Azam kuanzia 2020 hadi 2024.
Mshambuliaji huyo ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha kile alichokifanya Mayele yeye anakipiku licha ya kwamba rekodi zake za mabao zinamuhukumu kutokana na kutowahi kufikisha mabao 15 kwa msimu mmoja wala kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara.
Msimu ambao Dube ulikuwa bora zaidi kwake alifunga mabao 14, ulikuwa ule wa kwanza 2020-2021, baada ya hapo grafu yake ikawa inapanda na kushuka hadi anaondoka kikosini hapo.
Kennedy Musonda
Wakati Yanga inamsajili straika huyu kipindi cha dirisha dogo msimu wa 2022-2023, kutoka Power Dynamos ya Zambia, alikuwa kinara wa mabao 11 katika Ligi Kuu ya nchi hiyo, hivyo CV yake ilitarajiwa kumuongezea nguvu Mayele ambaye alikuwa kwenye kiwango kikubwa.
Msimu wake wa kwanza akisaidiana na Mayele kabla ya kutimka nchini alifanikiwa kutupia mabao mawili, aliyofunga dhidi Geita Gold na Dodoma Jiji.
Msimu wake wa pili ambao ndio ulikuwa wa mwisho kwake ndani ya Yanga, Musonda alifunga mabao manne dhidi ya JKT Tanzania, Simba na Mtibwa Sugar alipoifunga mara mbili. Hivyo jumla amefunga mabao sita katika ligi.
Dakika alizocheza na timu alizopambana nazo ni KMC (64), JKT Tanzania (78), Namungo (90), Geita Gold (17), Singida Fountain Gate (18), Simba (72), Coastal Union (59), Mtibwa Sugar (30), Tabora United (64), Kagera Sugar (34), Dodoma Jiji (61), Mashujaa (22), KMC (30), JKT Tanzania (80), Ihefu (60), Geita Gold (90), Simba (18), Coastal (90) na Mtibwa Sugar (90).
Hafiz Konkoni
Straika huyu alisajiliwa mwanzoni mwa msimu wa 2023-2024 akitokea Bechem United ya kwao Ghana ikiaminika anakuja kuziba pengo la Mayele ambaye ndiye alikuwa ameondoka kipindi hicho akiacha rekodi kabambe za mabao.
Konkoni ikaonekana amepewa mlima mrefu wa kuupanda, akashindwa kuendana na kasi inayotakiwa, akajikuta kipindi cha dirisha dogo akitolewa kikosini akiwa amefanikiwa kufunga bao moja katika Ligi Kuu.
Joseph Guede
Baada ya kasi ya Konkoni kushindwa kuendana na Yanga, uongozi wa timu hiyo ulifanya uamuzi wa kuongeza nguvu dirisha dogo la msimu uliopita kwa kumsajili Guede ambaye ameitumikia timu hiyo kwa miezi sita tu na kutupia mabao sita kwenye ligi.
Guede alianza kwa kusuasua kutokana na kushindwa kuzoea ligi lakini alionyesha uhai dhidi ya Musonda kwa kumzidi mabao mawili, yeye akitupia kambani sita huku Musonda akifunga manne.
Mshambuliaji huyo licha ya kuanza kuzoea ligi uongozi umeamua kuachana naye na kufanya maboresho kwa kumsajili Prince Dube na Jean Baleke. Swali ni je nani ataweza kuvunja ufalme wa Mayele?
Prince Dube
Ndiye mshambuliaji ambaye anatazamwa zaidi kwa sasa kutokana na uzoefu alionao kwenye Ligi ya Tanzania akihudumu kwa misimu minne ndani ya kikosi cha Azam FC.
Msimu wake wa kwanza ilikuwa ni 2020/21 akifunga mabao 14, msimu uliofuata hakuwa bora kwani alikaa sana nje ya uwanja kutokana na kupata jeraha la goti, alitupia bao moja tu.
2022/23 Dube akiwa na Azam FC alifunga mabao 12 na msimu wake wa nne na wa mwisho akicheza nusu msimu alitupia mabao saba kabla ya kuondoka kikosini na kuvunja mkataba na timu hiyo.
Sasa ni mali ya Yanga na anatajwa kuwa anaweza kuwa mshambuliaji tishio ndani ya kikosi hicho kutokana na uzoefu alionao ikiwa ni pamoja na kucheza sambamba na viungo wenye uwezo mkubwa.
Dube atakuwa katikati ya Clatous Chama, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki ambaye ndiye alikuwa kinara wa upachikaji mabao Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga mabao 21 na kumuacha mzawa Feisal Salum 'Fei Toto' aliyefunga mabao 18.
Dube afunguka
Mshambuliaji huyo amesema kazi yake ni kufunga, amesajiliwa na Yanga kwa ajili ya kazi hiyo, hivyo anaamini atakuwa na msimu bora baada ya kupata mapumziko ya muda na sasa anajiandaa kujiweka fiti kwa ushindani.
"Kila mchezaji anatamani kuwa kinara hasa ambaye anacheza eneo la ushambuliaji siwezi kuweka ahadi ya kufunga mabao mangapi, ni mapema sana ila nitafunga sana kwa sababu hiyo ndio kazi yangu," anasema na kuongeza;
"Kucheza pamoja na Chama, Aziz Ki na Pacome hakuna mchezaji ambaye hatamani kufanya kazi na wachezaji hao wenye uwezo mkubwa, nafurahi kuungana nao kwenye timu moja na naamini tutacheza kwa kushirikiana ili kuweza kuisaidia Yanga ifikie malengo."