Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Euro 2024- Ujerumani mambo yameiva

Munich, Ujerumani. Kipyenga cha fainali za mataifa ya Ulaya (Euro) 2024 kinapulizwa Ijumaa wiki hii kwa mchezo wa ufunguzi wa mashindano hayo utakaokutanisha mwenyeji Ujerumani na Scotland ukiwa ni mchezo wa kundi A utakaochezwa kuanzia Saa 4:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.

Baada ya kusubiri kwa miaka minne tangu fainali hizo zilipochezwa 2020, hisia za wapenzi na mashabiki wa soka duniani zinaelekezwa Ujerumani ambako maandalizi ya kuandaa fainali hizo yanaonekana kukamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na sasa kinachosubiriwa ni timu 24 kuwania taji la mashindano hayo mwaka huu.


Timu zipo kamili

Timu 24 zitakazoshiriki mashindano hayo mwaka huu ni wenyeji Ujerumani, Ubelgiji, Ufaransa, England, Ureno, Hispania, Croatia, Switzerland, Uturuki, Austria, Uholanzi, Hungary, Slovakia na Albania.
Nyingine ni Denmark, Romania, Serbia, Jamhuri ya Czech, Italia, Slovenia, Georgia, Ukraine, Poland na Scotland.

Ni mashindano ambayo hayatakuwa na baadhi ya timu zenye nyota wanaotamba Ulaya kwa sasa kama vile Sweden ya staa wa Newcastle United, Alexander Isack na Norway iliyo na nahodha wa Arsenal, Martin Odergaad na mshambuliaji kinara wa Man City, Erling Haaland.

Wageni katika mashindano hayo ni Georgia ambao watashiriki kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa wakati timu za Albania na Slovenia kila moja inashiriki kwa mara ya pili.

Timu ambayo kinara wa kushiriki mara nyingi fainali za Euro ni mwenyeji Ujerumani ambayo fainali za mwaka huu zitakuwa za 14 kwake ikifuatiwa na Hispania ambayo mwaka huu itakuwa inashiriki mara ya 12.


Makundi

Miamba hiyo 24 inayoshiriki fainali hizo mwaka huu imegawanywa katika makundi sita yenye timu nne kila moja ambapo kundi A litakuwa na Ujerumani, Scotland, Hungary na Switzerland wakati kundi B lina timu za Hispania, Croatia, Italia na Albania.

Timu zilizopangwa katika kundi C ni Slovakia, Denmark, Serbia na England wakati Poland, Uholanzi, Austria na Ufaransa zikiwa katika kundi D.
Katika kundi E kuna Ubelgiji, Slovakia, Romania na Ukraine na timu zilizopo katika kundi F ni Uturuki, Georgia, Ureno na Jamhuri ya Czech.


Waamuzi wa kutosha

Namba kubwa ya marefa itashuhudiwa wakichezesha fainali za mwaka huu kutoka nchi tofauti za Ulaya wakijumuishwa watatu kutoka Argentina ikiwa ni sehemu ya ushirikiano baina ya Uefa na Shirikisho la Mpira wa miguu Amerika Kusini, Conmebol.


Idadi ya marefa 

Kutakuwa na marefa 19 wa kati na wasaidizi wao 57, marefa watakaokuwa wakisimamia teknolojia ya video (VAR) ni 20 na pia 12 ambao watakuwa na jukumu la kuwapa usaidizi waamuzi watakaokuwa wakipangwa kwa mechi za mashindano hayo.

Marefa wa kati ambao wameteuliwa kuchezesha fainali hizo ni Jesús Manzano, Marco Guida,  István Kovács, Ivan Kružliak, François Letexier, Danny Makkelie, Szymon Marciniak, Halil Umut, Glenn Nyberg, Michael Oliver, Daniele Orsato, Sandro Schärer, Daniel Siebert, Artur Dias, Anthony Taylor, Facundo Tello, Clément Turpin, Slavko Vinčić na Felix Zwayer.

Waamuzi wasaidizi watakuwa ni Diego Sevilla, Ángel Rodriguez, Filippo Meli, Giorgio Peretti, Vasile Marinescu, Mihai Artene, Branislav Hancko, Jan Pozor, Cyril Mugnier, Mehdi Rahmouni, Hessel Steegstra, Jan de Vries, Tomasz Listkiewicz, Adam Kupsik, Mustafa Emre, Kerem Ersoy, Mahbod Beigi, Andreas Söderkvist, Stuart Burt, Dan Cook, Ciro Carbone
na Alessandro Giallatini.

Wengine ni Stéphane de Almeida, Bekim Zogaj, Jan Seidel, Rafael Foltyn, Paulo Soares, 
Pedro Ribeiro, Gary Beswick, Adam Nunn, Gabriel Chade, Ezequiel Brailovsky, Nicolas Danos, Benjamin Pages, Tomaž Klančnik, Andraž Kovačič, Stefan Lupp na Marco Achmüller.
Upande wa VAR kuna Stuart Attwell, David Coote, Jérôme Brisard, Willy Delajod, Bastian Dankert, Christian Dingert, Marco Fritz, Massimiliano Irrati, Paolo Valeri, Rob Dieperink na Pol van Boekel.
Pia wapo, Bartosz Frankowski, Tomasz Kwiatkowski, Catalin Popa, Nejc Kajtazovič, Tiago Martins, Alejandro Hernández, Juan Munuera, Fedayi San na Alper Ulusoy na watakaokuwa wakitoa sapoti ni Senad Ibrišimbegović, Aleksandr Radiuš, Johan Balder, Jan Erik Engan, Jure Praprotnik na Oleksandr Berkut.


Viwanja nyota tano

Kipute cha Euro 2024 kitapigwa katika viwanja 10 tofauti katika majiji mbalimbali ya Ujerumani ambapo mchezo wa ufunguzi utafanyika kwenye Uwanja wa Allianz Arena uliopo Munich na mechi ya fainali itachezwa katika Uwanja wa Olympiastadion jijini Berlin.

Ukiondoa hivyo viwili pia kuna viwanja vya Westfalenstadion (Dortmund), Stuttgart Arena (Stuttgart), Arena AufSchalke (Gelsenkirchen), Frankfurt Arena (Frankfurt), Volksparkstadion (Hamburg), Düsseldorf Arena (Dusseldorf), Cologne na Leipzig.


Macho kwenye taji

Ujerumani na Hispania zinashiriki fainali hizo mwaka huu kila moja ikiwa na kiu ya kutwaa taji ili iandike rekodi ya kuwa taifa lililotwaa mara nyingi zaidi ubingwa kwenye mashindano hayo.

Hadi sasa timu hizo kila moja imetwaa ubingwa mara tatu ambapo Ujerumani imechukua katika miaka ya 1972, 1980 na 1996 wakati Hispania imenyakua taji katika miaka ya 1964, 2008 na 2012.

Ufaransa na Italia kila moja imechukua ubingwa wa mashindano hayo mara mbili tofauti na timu ambazo zimetwaa ubingwa mara mojamoja ni Russia, Uholanzi, Czech, Denmark, Ureno, Slovakia na Ugiriki.

England inasaka taji la kwanza la mashindano hayo ili kufuta jinamizi baya ililonalo katika mashindano hayo ambayo mafanikio makubwa iliyowahi kuyafikia ni kufika hatua ya fainali mara moja ambayo ni mwaka 2020.