Prime
Fadlu na muendelezo wa nuksi Kariakoo Dabi
Muktasari:
- Kocha wa mwisho wa Simba kuifunga Yanga ni Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na baada ya hapo hakuna mwingine aliyeweza kuutafuna mfupa huo ambao unaonekana ni mgumu.
Jumatatu, Septemba 22, 2025 mkataba wa Simba na Fadlu Davids ulifikia tamati baada ya Kocha huyo raia wa Afrika Kusini kujiunga rasmi na Raja Casablanca ya Morocco ambayo aliinoa awali kabla ya kuja Tanzania.
Kocha huyo ameondoka akiwa amehudumu ndani ya timu hiyo kwa siku 444 tu na kurejea Raja ambako siku za nyuma alikuwa kocha msaidizi.
Kuondoka kwa Fadlu Davids na wasaidizi wake wanne kulitokea siku sita tu baada ya mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga ‘Dabi ya Kariakoo’ uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 16.
Katika mchezo huo, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Pacome Zouzoua na hivyo kutwaa Ngao ya Jamii, ushindi ambao kwa upande mwingine ulikuwa wa sita mfululizo dhidi ya Simba.
Hata hivyo kupoteza dhidi ya Yanga, sio sababu iliyomuondoa Fadlu Davids ndani ya Simba lakini imeendeleza historia ya baadhi ya makocha ambao maisha yao ndani ya klabu hizo mbili hayakuwa marefu mara baada ya Dabi ya Kariakoo kwa sababu tofauti.
Robertinho
Kocha wa mwisho wa Simba kuifunga Yanga ni Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na baada ya hapo hakuna mwingine aliyeweza kuutafuna mfupa huo ambao unaonekana ni mgumu.
Maisha ya Robertinho ndani ya Simba yalienda vizuri hadi Novemba 5, 2023 pale timu hiyo ilipokutana na kipigo kizito cha mabao 5-1 kutoka kwa Yanga katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa kwanza wa Ligi Kuu msimu wa 2023/2024.
Siku mbili baada ya kichapo hicho cha Yanga, uongozi wa Simba ulitangaza rasmi kuachana na Robertinho na msaidizi wake Corneille Hategekimana.
Baada ya Robertinho kuondolewa, aliyekuwa Kocha wa Makipa, Dani Cadena alipewa jukumu la kukaimu kwa muda nafasi ya Ukocha Mkuu akisaidiana na Selemani Matola.
Ernie Brandts
Mholanzi Ernie Brandts alikuwa miongoni mwa makocha vipenzi vya mashabiki wa Yanga kutokana na soka safi ambalo timu hiyo ilikuwa inalitandaza chini yake.
Aliiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 na aliipa pia taji la Ngao ya Jamii 2013.
Hata hivyo Desemba 25, 2013, Yanga ilifikia makubaliano na kocha huyo ya kuvunja mkataba wake ikiwa ni siku tatu baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa watani zao Simba.
Baada ya Brandts kuondoka, nafasi ya Ukocha Mkuu Yanga ilikaimiwa na Fred Felix Minziro.
Moses Basena
Mei 18, 2013 ni kipindi ambacho Kocha wa Simba Mganda Moses Basena hatakisahau katika maisha yake ya soka alipofungwa na Yanga bao 2-0.
Kupoteza kwa mechi hiyo ndiyo ilikuwa tiketi ya Basena kurudi kwao Uganda, Mganda Hamis
Kiiza na Mrundi, Didier Kavumbagu waliiongoza Yanga kupatikana wa tiketi ya Basena baada ya kila mmoja kutupia bao moja wavuni.
Baada ya matokeo hayo Simba iliamua kuachana na kocha huyo ingawaje ilipita siku kadhaa tangu kukutana na watani zao hao.
Marcio Maximo
Kwa sasa anainoa timu ya KMC lakini umaarufu wa jina lake hapa nchini ulianza alipokuwa akiinoa Taifa Stars.
Mkataba wake ulipomalizika na Stars, kocha huyo aliamua kurejea Brazil. Mwaka 2014 Yanga ilimpa ajira, alirudi nchini lakini wakati tayari soka la Bongo halikuwa rafiki tena kwake.
Kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Simba kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe, kilitosha kumpa tiketi Mbrazili huyo bila kujali historia yake ya soka nchini akifanya vizuri na Stars.
Dylan Kerr
Muingereza huyo kabla hakuweza kudumu ndani ya Simba baada ya kufungwa mabao 2-0 na Yanga mara mbili.
Uamuzi haukuchukuliwa kwa haraka bali mwishoni mwa safari yake ulikuwa ni kwenye
mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambapo Simba iliboronga na kutolewa mashindanoni.
Abdallah Kibadeni
Kocha na nyota wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni msimu wa 2012-13 alipewa majukumu ya kuifundisha Simba akisaidiana na Jamhuri Kihwelo 'Julio' ambaye pia aliwahi kuichezea Simba miaka ya nyuma.
Makocha hao hawakudumu ndani ya Simba baada ya kulazimisha sare na watani wao, Yanga ya mabao 3-3, ambapo Yanga ilianza kufunga mabao yote matatu kipindi cha kwanza huku Simba ikirudisha yote kipindi cha pili, mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.