Fei aitwa tena, aingia mitini
Muktasari:
- Katika barua ambazo zimevuja iliyoelekezwa kwa Feisal, Mei 16 alipokea barua ya malalamiko kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo ikimtuhumu kwa makosa mbalimbali ya kinidhamu.
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Feisal Salum kwa mara ya kwanza juzi aliitwa katika kamati ya sheria na nidhamu, lakini inadaiwa kuwa hatukutokea.
Katika barua ambazo zimevuja iliyoelekezwa kwa Feisal, Mei 16 alipokea barua ya malalamiko kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo ikimtuhumu kwa makosa mbalimbali ya kinidhamu.
Barua hiyo ilieleza; "Kama ilivyoainishwa kwenye hati ya mashtaka ambayo imeambatanishwa kwenye barua hii, unaelekezwa kuwasilisha utetezi wako juu ya tuhuma zinazokukabili ndani ya siku saba (7) tangu ya barua hii."
Barua hiyo pia ilimuelekeza Feisal kuhudhuria kikao cha kamati ya sheria na nidhamu kitakachosikiliza mashtaka dhidi yake mnamo tarehe 24 (juzi), Mei 2023 saa 4:00 asubuhi katika ofisi za klabu zilizopo Jangwani ukumbi wa mikutano.
"Ukiwa pamoja na mwakilishi wako (iwapo utapenda kuwa na mwakilishi), ili kukusikiliza wewe pamoja na mlalamikaji na kufanya maamuzi juu ya tuhuma zinazokukabili;
"Fahamu kwamba kushindwa kwako kuwasilisha utetezi wa maandishi dhidi ya tuhuma zinazokukabili ndani ya muda uliotajwa au kutokufika kwenye kikao kutafanya kamati iendelee na kikao bila kuwepo," ilieleza barua hiyo.
FEI AINGIA MITINI
Habari ambazo gazeti hili linafahamu kwamba mchezaji huyo juzi hajatokea na hakutoa taarifa yoyote ile na kamati hiyo iliendelea bila kuwepo kwa Feisal na kilichobaki alisikilizwa mlalamikaji.
Kitendo cha Feisal kutotokea, kamati itapitia malalamiko kisha itatoa adhabu kwa mchezaji huyo ambapo majibu hayo bado hayajatoka.