Fifa yaishusha daraja klabu ya Ligi Kuu ya Kenya kwa kununua mechi

Fifa yaishusha daraja klabu ya Ligi Kuu ya Kenya kwa kununua mechi

Muktasari:

  • Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) limeishusha daraja klabu ya Zoo FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL) baada ya kuikuta klabu hiyo ya Kericho na kosa la kupanga matokeo.

Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) limeishusha daraja klabu ya Zoo FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL) baada ya kuikuta klabu hiyo ya Kericho na kosa la kupanga matokeo.

“Kamati ya Nidhamu ya Fifa imebaini klabu ya Zoo FC inahusika na vitendo vya kupanga matokeo ya mechi za mpira wa miguu na mashindano….Hivyo, klabu ya Zoo FC inaondolewa katika msimu wa 2020/21 wa Ligi Kuu kama siku ya taarifa ya uamuzi,” inasema barua ya Kamati ya Nidhamu iliyosainiwa na mwenyekiti wake, Alejandro Piera.

“Kamati ya Nidhamu ya Fifa inaagiza kushushwa daraja kwa timu ya kwanza ya Zoo FC hadi Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.”

Kutokana na uamuzi huo, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limeiandikia barua klabu hiyo yenye makao yake makuu Kericho kuitaarifu kuhusu uamuzi huo wa kuishusha hadi daraja la kwanza.

“Tunawataarifu kuwa tumepokea mawasiliano kutoka Fifa ya Mei 4, 2021 kuhusu uamuzi wa Kamati ya Nidhamu dhidi ya klabu yenu dhidi ya makosa ya kupanga matokto ya mechi za mpira wa miguu na za mashindano.

“Kutokana na suala lililotajwa awali, FKF imeiondoa klabu yenu katika msimu wa mwaka 2020/21 wa Ligi Kuu na kuishusha Zoo FC hadi National Super League (NSL) kwa msimu wa mwaka 2021/2022,” alisema katibu mkuu wa FKF, Barry Otieno.