Figo amkosoa Ronaldo, asema ajifunze kwa Messi
Muktasari:
- Kauli ya kiungo, Joao Neves kusema Ronaldo ni sawa na wachezaji wengine kwenye kikosi cha Ureno imemuibua gwiji, Luis Figo akimtaja Messi.
Kauli ya kiungo, Joao Neves kusema Cristiano Ronaldo ni sawa na wachezaji wengine imeendelea gumzo katika mitandao na vyombo vya habari duniani, ikimuibua winga wa zamani wa timu ya taifa ya Ureno, Luis Figo.
Figo amemkosoa nahodha wa sasa wa timu hiyo, Ronaldo, akisema anapaswa kuboresha namna anavyoongoza wenzake ndani ya kikosi.
Gwiji huyo amesema anamuheshimu Ronaldo kwa mchango mkubwa alioutoa kwa taifa hilo kwa miaka mingi, lakini amehoji uwezo wake wa kuunganisha timu akiwa kiongozi hasa kutokana na umri wake na nafasi aliyonayo hivi sasa.
“Namuheshimu Cristiano kwa kila alichokifanya kwa nchi yetu. Ni gwiji wa Ureno na anapendwa na wengi, lakini nina mashaka kuhusu uwezo wake wa uongozi,” amesema Figo.
Amesema wakati wa fainali za Euro 2004, Ronaldo akiwa mchezaji mdogo kwenye kikosi cha Ureno, wachezaji wakubwa walimpa sapoti na kumsaidia kuonyesha uwezo wake uwanjani, jambo ambalo anasema sasa anatakiwa kulirudisha kwa wachezaji wenzake.
Figo ametoa mfano wa mchezo wa Ureno dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akidai Ronaldo alipaswa kumpa nafasi Bruno Fernandes ambaye alikuwa katika nafasi nzuri ya kufunga badala ya kuamua kupiga mwenyewe.
“Niliona Bruno akiwa kwenye nafasi nzuri zaidi na alikuwa akiomba pasi, lakini Cristiano aliamua kupiga na hakufunga. Hili si suala la kumlaumu Bruno kwa kuvuruga timu,” amesema.
Aidha, Figo amefananisha hali hiyo na timu ya taifa ya Argentina, akisema wachezaji na makocha wanavyomheshimu Lionel Messi si kwa sababu ya mafanikio yake pekee bali kutokana na namna anavyowafanya wenzake wajisikie kuwa sehemu ya familia.
“Kuwa na kipaji pekee haitoshi, tabia ni muhimu katika kila eneo la maisha. Ronaldo anapaswa kujifunza kutoka kwa Messi kuhusu namna ya kuwaunganisha wachezaji,” amesema Figo.
Kauli hiyo imekuja baada ya mjadala kuibuka kuhusu uongozi wa Ronaldo ndani ya kikosi cha Ureno, huku kiungo Bruno Fernandes akiongeza mjadala baada ya kuonyesha kuunga mkono baadhi ya maoni yaliyohusishwa na ukosoaji huo kupitia mtandao wa Instagram.
Hata hivyo, kauli hiyo imempelekea kiungo Joao Neves kupoteza wafuasi wake katika mtandao wa Instagram kutoka milioni 5 mpaka milioni 3.
Kiungo huyo akizungumza wakati wa mahojiano na moja ya chombo cha habari baada ya mchezo dhidi ya DR Congo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 alisema Ronaldo ni mchezaji kama wengine na yupo kusaidia timu.
“Tunajua kile Cristiano amefanya kwa taifa letu na kwa soka duniani. Lakini kwa sasa, yeye na sisi tunajua kwamba yeye si tofauti. Ni mchezaji kama wengine hapa, yupo kusaidia timu. Hana tofauti na wengine,” alisema Neves.