Ghana v Nigeria: Mpambano unaogonga vichwa Kombe la Dunia Afrika

Muktasari:

  • Kama kuna mechi inazungumziwa sana kuliko nyingine nne za hatua ya mwisho ya kupata wawakilishi wa Afrika katika fainali za Kombe la Dunia, basi ni Ghana dhidi ya Nigeria, wababe wawili wa Afrika Magharibi wanaokutana Ijumaa katika mechi ya kwanza kati ya mbili.


Kama kuna mechi inazungumziwa sana kuliko nyingine nne za hatua ya mwisho ya kupata wawakilishi wa Afrika katika fainali za Kombe la Dunia, basi ni Ghana dhidi ya Nigeria, wababe wawili wa Afrika Magharibi wanaokutana Ijumaa katika mechi ya kwanza kati ya mbili.

Timu zote mbili zimewahi kufuzu kucheza fainali hizo kubwa katika mchezo wa soka na hazijaweza kuvuka hatua ya robo fainali, Ghana ikipoteza nafasi ya wazi kufika nusu fainali mwaka 2010 wakati Asamoah Gyan alipokosa penati katika dakika za mwisho za mechi dhidi ya Uruaguay, penati iliyotolewa baada ya Luis Suarez kuudaka kwa makusudi mpira wa kichwa wa Dominic Adiyiah uliokuwa ukielekea wavuni.

Suarez, aliyeonyeshwa kadi nyekundu baada ya tukio hilo na kutakiwa kwenda vyumba vya kubadilishia nguo, alisimama kushuhudia penati hiyo na baada ya Gyan kupaisha, aliruka kwa furaha na kukimbilia vyumbani.

Wawili hao wanakutana safari hii kuamua mbabe baina yao katika miaka ya karibuni, huku timu zote zikitoka fainali za Mataifa ya Afrika nchini Cameroon na rekodi mbaya, Nigeria ikitolewa katika raundi ya 16 bora na Tunisia, huku Ghana ikitolewa kwa aibu katika makundi, ikiwa haijashinda mchezo hata mmoja.

Na hali hiyo, ukichanganya na majeruhi, kadi na timu kutokuwa katika ubora wake, kunaifanya Ghana iingie katika mechi hizo mbili ikitegemea zaidi historia na nguvu za nje ya uwanja.

Baada ya kusitasita kuamua mchezo ufanyike wapi, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limeamua mechi hiyo ichezwe jijini Kumasi, sehemu ambako kumekuwa machinjio ya timu wakati wa mechi muhimu.

Ikijua kuwa haitakuwa na Asamoah, ambaye pia hakwenda Cameroon katika fainali za Afcon, hali kadhalika Andrew Ayew, ambaye amekuwa nyota wa timu hiyo katika miaka ya karibuni na atakayekosekana kutokana na kuwa na kadi, Ghana haionekani kuwa na timu imara mbele ya Nigeria yenye nyota wengi wanaosakata soka katika klabu kubwa Ulaya.

Itamtegemea zaidi Thomas Partey, ambaye katika siku za karibuni amekuwa aking'ara na Arsenal na kuiongoza katika kujikita katika nafasi nne za juu za Ligi Kuu ya England. Pia yumo Daniel Amartey (Leicester City) katika kikosi hicho, huku Jordan Ayew aliyekuwa na maambukizi ya Covid-19, ameripotiwa kupona na amejiunga na kikosi hicho.

Lakini Ghana ina nguvu nyingine kwa wachezaji watakaotaka kuthibitisha ubora wao katika mechi kubwa.

"Nyota Mohammed Kudus, ambaye kipaji chake kinaonekana kuwa kizuri katika mechi kubwa, hana sehemu nyingine nzuri ya kukionyesha kuliko katika mchezo dhidi ya wapinzani wao wa jadi ambao ni Nigeria," imeandika supersport.com.

Bila ya wawili hao, wachezaji wengine katika timu hiyo ya kocha Addo Otto ni wale wasio na majina na ambao mashabiki wa soka wa Ghana hawana imani nao kubwa kuwa wanaweza kufurukuta mbele ya Nigeria.

Na tovuti hiyo imeandika kuwa ujumbe pekee kutoka kwa kocha Addo Otto kwa wachezaji waliosalia umekuwa ni "huu ni wakati wenu kuandika historia yenu".

Ni kutokana na hali ya timu kwa sasa, hata jiji la Kumasi litakuwa muhimu kwa timu kujiongezea nguvu za ziada kuikabili Nigeria. Katika uwanja wa Baba Yara jijini Kumasi ndiko Misri ilipocharazwa mabao 6-1 wakati Ghana ilipofuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, ikishinda mechi zake zote za nyumbani.

Wakati ikielekea fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, Ghana ilitumia jiji hilo kushinda mechi mbili kati ya tatu na wakati ikifuzu kwa mara ya kwanza mwaka 2006 ilishinda mechi tano kati ya sita za nyumbani.

Kumasi ni jiji ambalo wakazi wake wanapenda kwenda uwanjani kuishuhudia timu ya taifa.

"Jiji lina utamaduni mzuri wa mashabiki kuishabikia timu yao bila ya kujali matokeo. Na hicho ndicho Nigeria inaweza kukabiliana nacho Ijumaa, ambacho kitatosha kutoa matokeo mazuri kabla ya mechi ya marudiano," inaandika supersport.com.

Pamoja na faida ya kuchezea jijini Kumasi, Ghana itategemea hamu ya pamoja, nia, vipaji na maajabu ya mechi za wakubwa wa eneo moja kuweza kupata matokeo mazuri katika mchezo huo.

Addo atakuwa akiiongoza Ghana kwa mara ya kwanza baada ya kutimuliwa kwa kocha Mserbia, Milovan Rajevac kutokana na matokeo mabaya ya fainali zilizopita za Afcon. Addo atasaidiwa na kocha wa zamani wa Newcastle na Brighton, Chris Hughton.

Nigeria ina nafasi kubwa

Nigeria inapewa nafasi kubwa ya kuiondoa Ghana katika hatua hiyo licha ya rekodi kuonyesha kila timu imewahi kushinda mara mbili katika michuano ya awali ya Kombe la Dunia, huku mechi nyingine nne zikiisha kwa sare.

Nigeria inajivunia kikosi kipana zaidi ya ilichokuwa nacho katika fainali za Cameroon, huku safari hii washambuliaji kama Emmanuel Dennis, Odion Ighalo na Victor Osimhen wakiwemo kikosini, ingawa kipa nambari moja, Maduka Okoye hatakuwemo kutokana na kuugua na kiungo Wilfred Ndidi ameeumia.

Nafasi ya Okoye imechukuliwa na kipa wa Enyimba, John Noble.

Nigeria iko chini ya makocha wawili, Augustine Eguavoen, aliyeiongoza timu fainali za Afcon nchini Cameroon, na winga wa zamani wa nchi hiyo na Barcelona, Emmanuel Amuneke. Wawili hao wana tabia tofauti, Eguavoen akiwa muungwana mwenye kuruhusu wachezaji kutoa maoni yao, huku Amuneke akiwa mkali na mwenye kutaka kusikilizwa.

Taifa hilo lina kila mchezaji ambaye kocha angetamani kuwa naye.

Nahodha Ahmed Musa na msaidizi wake, William Ekong walikuwa miongoni mwa wachezaji 18 walioripoti kambini Jumatano.

Nigeria, meanwhile, also possess elite talent Pia itaelekeza nguvu zake kwa Ademola Lookman (RB Leipzig), Kelechi Iheanacho (Leicester City) na Victor Osimhen (Napoli). Osimhen pekee amefunga mabao manne ya michuano hiyo na atakuwa tishio kwa ngome ya Ghana.

Kabla ya kufungwa bao 1-0 na Tunisia na kuondolewa fainali zilizopita za Afcon, Nigeria ilikuwa haijapoteza mechi sita, ikitoka sare moja na kushinda tano zikiwemo tatu za matua ya makundi nchini Cameroon.

Hivyo itakuwa ikitaka kurejea katika wimbi la ushindi dhidi ya timu ambayo imekuwa ikiisumbua katika siku za hivi karibuni, ikiwa imepoteza mechi tatu na sare moja tangu ipate ushindi wa bao 1-0 mwaka 2006.

Mechi nyingine za hatua ya kufuzu za Kombe la Dunia zinazochezwa Ijumaa barani Afrika ni:

Cameroon           v Algeria

DR Congo            v Morocco

Mali                       v Tunisia

Misri                      v Senegal