GSM kujenga uwanja mpya wa Yanga
Muktasari:
- Mchakato wa kupitia maombi ya tenda za kuomba kugharamia na kujenga Uwanja wa Yanga, umefanyika kwa muda wa siku 14.
Yanga imeitangaza Kampuni ya GSM Limited kuwa mshindi wa tenda ya ubia wa ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo katika eneo la Jangwani, Dar es Salaam.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kmawe amesema kuwa kampuni hiyo ndio imeonekana kuwa na sifa stahiki za kuibuka mshindi kati ya nyingi zilizoomba tenda hiyo.
"Na nikiri tulipata maombi mengi kutoka taasisi na kampuni mbalimbali. Tuliendesha mchakato kwa weledi mkubwa. Tuliweka pia vigezo. Baada ya kutoa vigezo vile na maombi kutumwa kwa wingi, tukawa na siku 14 za kuchakata ni nani amekidhi vigezo.
"Jumamosi viongozi wa kamati ya utendaji walikutana na kuchakata maombi na niwajulishe kuwa kampuni ya GSM Limited, imeibuka mshindi wa tenda ya ubia wa kujenga uwanja wetu," amesema Kamwe.
Kamwe amesema kuwa kinachofuata baada ya mshindi wa tenda kutangazwa ni kukutana kwa uongozi wa Yanga na kampuni hiyo hiyo ili kujadili mambo mawili ya msingi.
"Kuna mambo mawili hapa ambayo yanafanya pande hizi mbili kukutana. Jambo la kwanza ni la kisheria. Hili linahusisha sheria hivyo viongozi wetu wanaenda kupata muongozo wa kisheria.
"Pili jambo hili linahusisha biashara. Huyu anamiliki ardhi na kuna anayetoa fedha," amesema Kamwe.
Kamwe alisema kuwa kuna kamati iliyoundwa ambayo ndio itakutana na kampuni iliyoshinda tenda ya ubia wa kujenga uwanja huo ili kujadili mambo hayo mawili.
Kamati hiyo inaongozwa na Mwenyekiti Hersi Said ambaye ni Rais wa Yanga na inaundwa na wajumbe wa Kamati ya utendaji ya klabu pia ikiwa na Mwanasheria Alex Mgongolwa na Mtaalam wa masuala ya biashara, Ivan Tarimo.
Ikumbukwe, Januari 9, 2026, Yanga ilitangaza fursa kwa kampuni na taasisi mbalimbali kuomba ushirikiano wa ubia wa kujenga uwanja wa klabu hiyo eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam.
Yanga ilitaja mambo nane ambayo ya msingi ambayo waombaji husika wanatakiwa waihakikishie klabu mojawapo ni kuwa na uwezo wa kujenga uwanja unaoingiza idadi ya watu 25,000 hadi 35,000.