Prime
MZEE WA FACT: Siku kama hizi tuliziona ndotoni tu
Muktasari:
Soma zaidi hapa...
Ni wikendi ya mwisho ya Januari inayoungana na ya kwanza ya Februari, 2026.
Mashindano ya vilabu barani Afrika yako katika hatua ya makundi, mzunguko wa nne.
Tanzania kama nchi pekee Kusini kwa Jangwa la Sahara kutoa wawakilishi wanne, inashuhudia timu zake tatu zikiwa uwanjani.
Lakini hiyo sio kubwa sana kwa sababu tangu zilipofuzu hatua hii, hiyo imekuwa kawaida toka mzunguko wa kwanza wa hatua ya makundi hadi sasa.
Kubwa ni kwamba timu tatu kati ya nne ziko nyumbani...nchi imechangamka.
Yanga waliwakaribisha Al Ahly kutoka. Misri, uwanja wa Amaan Zanzibar.
Simba dhidi ya Esperance ya Tunisia uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.
Azam FC wenyeji wa Nairobi United ya Kenya uwanja wa Amaan Zanzibar.
Hizi ni nyakati ambazo kama nchi tumekuwa tukizitamani kwa muda mrefu sana.
Tuliishia kuziona kwa wenzetu huku sisi tukiziota.
Ndipo unapokuja wimbo wa Nandy, Sugar, siku kama hizi tuliziona ndotoni tu. Kidogo siku hizi na sisi tuna nafuu.
Unaangalia mashindano mbalimbali unaona nchi fulani ina timu kibao hadi zinakutana zenyewe kwa zenyewe.
Kama ilivyokuwa kwa FAR Rabat na Raja Casablanca walipokuwa pamoja kundi C la ligi ya mabingwa msimu wa 2024/25.
Nchi moja kutoa timu nyingi hadi kukutana zenyewe ni moja ya matukio ya kuvutia sana kwenye mashindano.
Tanzania kama nchi tuliishia kuona wenzetu wakifanya hivyo.
Japo Tanzania hatujakutanisha timu zetu kwenye haya mashindano, lakini msimu bado unaendelea na yawezekana huko mbele zikakutana.
Na hata zisipokutana, kuwa na wikendi kubwa kama hii ni jambo la kukumbukwa sana. Ni tamu asali. Ni tamu hatari. Ni tamu sana.
Timu za nchi moja kukutana kwenye mashindano ya CAF ilianza mwaka 2005 pale wababe kutoka Tunisia, Esperance Tunis na Étoile Sportive du Sahel, walipokutana.
Ikajirudia tena mwaka 2008 pale mahasimu wa Cairo, Al Ahly na Zamalek walipopangwa pamoja kundi A.
Mwaka 2009 ikawa zamu ya wana CECAFA wenzetu, Sudan, pale wababe wawili wa Khartoum, Al Hilal na Al Merreikh, walipojikuta pamoja kwenye kundi.
Misri ikarudi 2010 kukutanisha timu mbili kwenye mashindano ya Afrika pale Al Ahly na Ismailia walipokutana kwenye kundi B.
2012 Tunisia ikarudi tena kwa Esperance Tunis na Etoile Sahel kukutana tena kwenye kundi A.
Al Ahly na Zamalek wakakutana tena 2013 kwenye kundi A.
Mwaka 2014 ndio ulikuwa babu kubwa. Nchi mbili tofauti zilitoa timu za kukutana kwenye mashindano.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliwakutanisha TP Mazembe na AS Vita Club kwenye kundi A.
Na Tunisia iliwakutanisha Esperance na CS Sfaxien kwenye kundi B.
Kama 2014 ilikuwa babu kubwa, basi 2015 ilikuwa zaidi na zaidi.
Mwaka huu timu tatu za nchi moja zilikutana kwenye kundi moja.
Nchi hiyo ni Algeria ambayo iliwakutanisha wanabe wake Es Setif, USM Alger na MC El Eulma kwenye kundi B.
Hii ilisababisha CAF kubadilisha sheria na kukataza timu zaidi ya mbili kutoka nchi moja kushiriki mashindano ya aina moja.
Mwaka 2017 pale hatua ya makundi ilipopanuliwa na kuwa na timu 16 kutoka timu 8.
Al Hilal na El Merreikh za Sudan zikakutana tena kwenye kundi A.
Hata hivyo FIFA iliifungia Sudan na kusababisha timu hizo kushindwa kumalizia mechi zao.
2018 MC Alger na ES Setif za Algeria zikakutana kundi B. Msimu wa 2021-22 ulikuwa hatari zaidi yq SUGAR ya Nandy.
Makundi matatu yalishuhudia timu za nchi moja zikikutana.
Kundi A lilikutanisha wababe wa Khartoum Sudan, Al Hilal na Al Merreikh.
Kundi C, Esperance Tunis na Etoile Sahel za Tunisia ziliminyamana kibabe.
Na kundi D lilikutanisha timu kutoka Angola, Petro Luanda na Sagrada Esperanca.
ILITUUMA SANA
Licha ya machafuko, Sudan wameshakutanisha timu zao mara kadhaa. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tayari. Angola nao tayari...bado sisi.
Hii hatua ambayo tumeifikia ya kuingiza timu nyingi ni dalili, ipo siku tutashuhudia timu zetu zikikutana na kutuandikia historia mpya.
Pata picha Yanga na Simba wapo kundi moja, halafu ratiba inawakutanisha kwenye mechi za pika pakua.
Yaani mechi ya tatu na nne ambazo asili ya kucheza na kurudiana hapo hapo...kama Simba na Esperance au Yanga na Al Ahly.
Msisimko wake utakuwa wa hali ya juu sana.
Lakini wakati tukiendelea kusubiri siku kama hizo, tuendelee kufurahia siku kama hizi tulizonazo sasa.
Afrika iko Tanzania. Esperance ni moja ya timu kubwa sana Afrika...Al Ahly hali kadhalika.
Zote zipo Tanzania siku kama hizi tulikuwa tukiziona ndotoni tu!