Prime
MZEE WA FACT: Unafiki wa FIFA
Februari 24, 2022, Urusi iliivamia kijeshi Ukraine na kusababisha mgogoro mkubwa unaoendelea hadi sasa.
Februari 28, 2022, siku nne tu baadaye, FIFA ikachukua hatua kali na za haraka dhidi ya Urusi.
Urusi ikafungiwa uanachama wa FIFA na UEFA. Timu yake ya taifa ikaondolewa kwenye mchakato wa kufuzu Kombe la Dunia na vilabu vyake vikaondolewa kwenye mashindano ya Ulaya, Urusi ikatengwa!
Januari 3, 2026, Marekani imeivamia Venezuela na kumteka rais wao na kwenda naye Marekani na kumshitaki kwenye mahakama yao. Hili ni tukio baya zaidi ya lile la Urusi, lakini FIFA hadi sasa iko kimya. Haijasema chochote hadi sasa, zaidi ya juma moja kupita.
Ililichukua shirikisho hilo la kimataifa siku nne tu kuiadhibu Urusi, lakini sasa inakaribia majuma mawili, hakuna dalili za kuiadhibu Marekani.
Hali hii inatokea katika wakati ambao dunia inaelekea kwenye mashindano makubwa zaidi ya soka, Kombe la Dunia, yatakayofanyika katika nchi tatu za Amerika Kaskazini; Marekani, Canada na Mexico.
Kama wangekuwa sio wanafiki, FIFA walipaswa kufanya kama walivyofanya 2022 kwa Urusi, kuifungia Marekani, kuitenga na hata kuipoka uenyeji wa Kombe la Dunia.
Au watoke hadharani waseme mwaka 2022 walikosea kuchukua hatua zile dhidi ya Urusi. Waifungulie na waombe radhi na kufidia hasara zote ambazo Urusi ilipata kwa kufungiwa na kutengwa.
Kukaa kimya kama hakuna kilichotokea ni unafiki mkubwa sana kwa shirikisho hilo ambalo hupaswa kuwa na msimamo wa katikati kwenye masuala yote yasiyo ya kimichezo, bila kuegemea upande wowote.
Kwa mujibu wa kanuni zake, FIFA haitakiwi kujihusisha na mambo ya kisiasa na hutakiwa kuwa na msimamo wa kutofungamana na upande wowote.
Hii ni pamoja na kuzuia uingiliaji wa serikali kwa mambo binafsi ya vyama wanachama wake kupitia vipengele vya katiba yake kama ibara 2(2) na 15(c).
Hata hivyo, licha ya kanuni kuizuia kujihusisha na siasa na kuchagua upande, FIFA kama nilivyosema hapo juu, ilijihusisha na siasa kwa kuifungia Urusi.
Lakini ikashindwa kuchukua hatua dhidi ya Israel kwa kuivamia Palestina na sasa Marekani kwa kuivamia Venezuela.
Mambo muhimu kuhusu FIFA & Siasa
Uhuru wa kikatiba: Sheria za FIFA zinataka vyama wanachama wake kuwa huru dhidi ya uingiliwaji na ushawishi wa mamlaka zingine (serikali), uvunjivu wa sheria hii adhabu yake ni kufungiwa.
Utekelezaji & Kukosa Muendelezo: Japo vyama wanachama vyapaswa kuwa huru, FIFA ilizifungia nchi kama Urusi mwaka 2022, kwa sababu za kisiasa, ikidhihirisha unafiki wake na kujitoa katika hali ya kutochagua upande wowote.
Siasa za muandaaji mashindano: Kuandaa Kombe la Dunia, FIFA mara kadhaa imejikuta katikati ya jicho kali la kisiasa, ikishinikizwa kuzingatia mambo ya kisiasa kama haki za binadamu, sheria za kazi, na uhuru wa kutoa maoni na kujieleza katika nchi waandaaji kama ilivyokuwa Qatar na sasa Marekani.
Muktadha wa kihistoria:
FIFA ina historia ya kujizima data kwa mambo ya kisiasa pale inapotaka kufanikisha jambo lake hasa Kombe la Dunia, kama ilivyokuwa Argentina 1978.
UNAFIKI UNAFIKI UNAFIKI
FIFA ilipiga marufuku mabango ya mashabiki yenye ujumbe wa Free Palestine wakati wa Kombe la Dunia la Qatar 2022, lakini ikaruhusu mabango ya kutangaza mambo mengine ya hovyoo.
Kwa miaka mingi sana ulimwengu wa michezo ulikaririshwa kwamba siasa hazituhusiwi michezoni. Japo tunajua kwamba siasa inatawala asilimia zaidi ya 60 ya kila kitu duniani, lakini michezo ilijifanya kutaka kujitenga nayo.
Japo wanasiasa waliendelea kuwa marafiki wakubwa wa michezo na wanamichezo wakiwemo viongozi wa taasisi za kimichezo kama FIFA, lakini siasa ilitajwa kuwa adui.
Kwenye AFCON ya 2008 nchini Ghana, Mohamed Aboutrika wa Misri alifunga bao dhidi ya Sudan na kuvua jezi yake ili aoneshe ujumbe wa kisiasa wenye mlengo wa huruma kwa watu wa Gaza, Palestina.
Itakumbukwa mzozo wa miaka yote wa Israel na Palestina na wiki hiyo Israel ilifunga mipaka ya Gaza na kusababisha mtafaruku kwa sababu watu wa mji huo hutegemea mahitaji yao kutoka nje, hasa Misri. Kitendo cha Israel kuwafungia ndani kililenga kuwaua njaa.
Watu zaidi ya laki saba wakakiuka vizuizi vile na kuingia Misri kununua mahitaji yao ya msingi kama chakula.
Ndipo Aboutrika akatoa ujumbe kwa dunia kuwaonea huruma watu wa Gaza, Sympathize With Gaza’, ndivyo fulana yake aliyoivaa kwa ndani ilivyosomeka. Aboutrika aliandikiwa barua rasmi na CAF, ya onyo kali sana.
CAF wakasema FIFA inakataza sana ujumbe wa kisiasa kwenye michezo. Afrika ikamezeshwa hivyo, na dunia ikaamini hivyo.
Kwenye kombe la dunia 2018, kocha msaidizi wa Croatia, Ognjen Vukojevic, alifukuzwa kazi wakati mashindano yakiendelea, kwa kosa la kuweka kwenye mtandao wa kijamii video fupi yenye ujumbe wa kisiasa akiwa mchezaji wake, Domagoj Vida. Vida mwenyewe ambaye ndiyo aliongea kwenye video hiyo akapewa onyo kali.
Ujumbe ulikuwa siasa haziruhusiwi kwenye mpira. Lakini zikaruhusiwa kwa Urusi. Sheria huleta maana pale inapokuwa msumeno, kwamba inakata mbele na nyuma.
Lakini tofauti na hivyo, hiyo sio sheria bali ni zana ya kunyamazisha wengine na kuwapa uhuru wa kufanya chochote wengine.