Guardiola amtolea uvivu Grealish

Manchester, England. Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amesema haridhishwi na kiwango duni kinachoonyeshwa na Jack Grealish akimtaka abadilike vinginevyo atasotea benchi.
Mchezaji huyo ameichezea Manchester City mechi 14 za Ligi Kuu England (EPL) msimu huu akiwa hajapachika bao lolote na amepiga pasi moja tu ya mwisho hadi sasa.
Manchester City ilitumia kiasi cha Pauni 100 katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi, 2021 kumnasa Grealish ikitegemea angekuwa na mchango mkubwa katika kikosi chao hasa baada ya kukoshwa na kile alichokifanya akiwa na Aston Villa.
Hata hivyo mchezaji huyo ameshindwa kujihakikishia namba na hilo limemfanya Guardiola ajitokeze hadharani na kumkumbusha m kuwa anatakiwa kutoa kitu kikubwa zaidi kwenye timu kuliko afanyavyo.
Guardiola amesema kuwa Grealish amekuwa hana mchango mkubwa kwa timu kulinganisha na wachezaji wengine wa nafasi ya winga hivyo wakati umefika sasa kwake kuboresha zaidi kiwango ili awe na msaada mkubwa kwa timu.
Alisema kuwa anatamani kumuona mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29, akifanya mambo makubwa kama ambayo ilivyokuwa katika siku za mwanzoni alipojiunga nao.
Kocha huyo alisema ni ngumu kwa Jack Grealish kupata muda mwingi wa kucheza mbele ya Savinho ambaye amekuwa akionyesha kiwango cha kuvutia.
“Ninamtaka Jack ambaye alishinda mataji matatu. Nahitaji hicho lakini niwe mkweli kwa hilo. Kilichotokea kwa Savinho kwenye ile krosi? Ni juu kuliko winga yeyote kwenye nafasi yake.
“Kwa vile anajiangalia yeye mwenyewe, ataona ushindani. Anatakiwa pia ashindane na yeye mwenyewe. Savinho yuko vizuri na ana kila kila kitu kuliko Jack (Grealish) na ndio maana ninamchezesha Savinho,”alisema Guardiola na kwamba kama Grealish asipobadilka, asitegemee kuwa atapata nafasi ya kucheza katika kikosi chake kwa huruma kwani anahitaji mchezaji anayweza kuipa timu kitu ndani ya uwanja.
“Wanatakiwa kupambana kila siku. Apambane. Hakuna suala hata la kujiongeza hapa. Unaweza kusema sawa, sio haki. Kama unafikiria hivyo ni sawa pia. Lakini unatakiwa kuthibitisha,” alisema.
“Nitaendelea kupambana nikiwa na Savinho kwamba anastahili kupata nafasi ya kucheza kwenye hiyo nafasi. Kila siku moja, wiki moja na kila mwezi mmoja.”
Na wakati Manchester City ikikaribia kumsajili Omar Marmoush kutoka Eintracht Franfurt ambaye pia anaweza kucheza winga, Guardiola alisema kuwa Grealish anatakiwa akaze buti vinginevyo atasotea sana benchi.
“Ninajua anaweza kwa sababu niliwahi kumuona, najua daraja lake na ninalitaka katika kila mechi, nyakati za mazoezi na katika kila mechi. Kuna mtu yeyote ambaye anahisi Savinho hastahili kucheza hivi sasa? Hapana anastahili ndio maana namchezesha kwa sababu anazalisha.”