Haitakuwa huru kama haina uhuru

Mbeya. 2007 wadau wa soka walikutana Bagamoyo katika mipango ya kuhakikisha soka letu linaendeshwa katika mfumo wa kisasa ili liweze kupiga hatua.

Azimio la Bagamoyo lililenga kufanya soka letu liwe kisasa, zamani viongozi wote hadi katibu mkuu, ofisa habari na hadi mweka hazina walikuwa wanachaguliwa.

Azimio lile likalenga kuunda sekretarieti kwenye klabu ili kuondoa ile hali ya klabu kuyumba kila baada ya uchaguzi. Pia kuliwekwa viwango vya elimu ya mpira kwa wale wanaokaa benchi la ufundi.
Ni katika kutaka kuufanya mpira wetu uendeshwe kisasa, ndipo ikaonekana hata ligi haina budi kuendeshwa na wanaoicheza badala ya chama cha mpira.

Lengo lilikuwa ni kutaka wanaoucheza waisimamie ligi bila ya kupendeleana na kwa haki kwa kuwa kikiwepo chombo juu yao kisichotokana na wao wenyewe, uwezekano wa kutowajibika ipasavyo kwa wenye ligi ukawa mdogo.

Ndipo TFF ilipoziagiza klabu zikutane na kuunda chombo chao. Lakini viongozi wa klabu wakashindwa kukutana hadi mwaka 2012 wakati TFF ilipoulizia maendeleo ya kuundwa kwa chombo hicho.

Lakini viongozi wakasema wameshindwa kwa kuwa kila wanapoitana, hakuna anayeibuka na kumuomba rais wa wakati huo, Leodegar Tenga aanzishe mchakato mwenyewe.

Tenga akaunda kamati ya ligi ambayo lengo lake lilikuwa ni kushughulia kuanzishwa kwa Bodi ya Ligi. Kamati ilijumuisha viongozi wa klabu nyingi za Ligi Kuu na TFF ikabakia na kuunda mwongozo wa mahusiano (governing regulations) baina ya TFF na bodi ya ligi.

Kazi kubwa ya TFF ibakie katika program za maendeleo na zile za kisera. Timu za taifa zote zinatakiwa zishughulikiwe na TFF, mafunzo kwa waamuzi, viongozi, madaktari wa michezo, makocha ndiyo kazi za TFF.

Mashindano ya vijana, watoto na wanawake ndio kazi kuu ya TFF kama ambavyo unaona jinsi FA ya England isivyojiingiza kwenye Ligi Kuu kwa namna yoyote ile.
 

Kwa nini TPLB si huru

Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo anasema huo ni mtazamo na siku zote, safari ni hatua na inawezekana watu wanazungumza hivyo sababu haiakisi moja kwa moja kila wanachomanisha.

"Ni kweli Bodi ya Ligi si taasisi inayojitegemea moja kwa moja, lakini ukitazama jinsi inavyofanya kazi inafanya kama taasisi iliyokuwa huru kwa kufuata miongozo tuliyokuwa nayo.

"Governing Regulations ndiyo dira ya TPLB, hivyo kusema kwamba si huru hilo nakataa, kwa sababu haiakisi ule uhalisia ambao sisi tuliokuwa nao," anasema Kasongo.

Anaongeza kwamba watu wanachanganya mambo katika kutafisri uhuru wa TPLB lakini uhuru waliokuwa nao ni mkubwa kiasi kwamba maamuzi yao wanayofanya kuhusu ligi hayaingiliwi na chombo chochote labda mtu aende CAS au Caf.

Katibu mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah anasema kwanza ukiangalia tu waajiriwa wanapatikanaje. Mtendaji Mkuu wa TPLB ameajiriwa na TFF, na inawezekana wafanyakazi wote wa TPLB ni waajiriwa wa TFF.

"Kifupi huwezi kwenda TPLB bila ya ridhaa ya TFF. Ni nani anaunda kanuni. 'Governing regulations' zinataka TPLB ndiyo iunde kanuni za ligi na kazi ya Kamati ya Utendaji ya TFF ni kuzipitisha tu.

Hivi sasa, mwenyekiti wa TPLB hawezi kuitisha kikao chochote bila ya ridhaa ya TFF. Makosa yanayofanyika kwenye Ligi Kuu na Ligi ya Championship yanashitakiwa na TFF badala ya TPLB kuyapeleka kwa kamati huru za TFF, kama kamati ya nidhamu au ya maadili.

Aliyekuwa Mtendaji wa TPLB, Boniface Wambura aliwahi kusema akiwa madarakani kuwa inategemea mtu anazungumzia uhuru upi wa bodi, kwa maana ya wengi wanashindwa kuelewa muunganiko wa Bodi na TFF, kwa sababu kuna katiba TFF na kanuni za uendeshaji wa mashindano, hivyo kuna mamlaka yapo TFF na mamlaka yapo TPLB.

"Masuala yote yanayohusiana na waamuzi, nidhamu na maadili yapo TFF, hivyo mtu akifanya kosa lanalohusu nidhamu, bodi inampeleka TFF kwasababu wao hawana mamlaka ya kumuhukumu, japo kuna marekebisho ambayo yamefanyika, ndiyo maana kuna kamati ya masaa 72 inayofanya kazi haraka," anasema Wambura.

Alisema dhana ya uhuru ni pana na kuongeza ndio maana watu husema hakuna uhuru usiokuwa na mipaka na kwa kufanya hivyo inaleta uwiano mzuri.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Ndimbo anasema Ligi Kuu na Ligi ya Championship zote zipo chini ya TPLB na wanafanya kazi yao bila kuingiliwa na mtu.

"Kama wao wanasimamia na kuendesha ligi hapo unahitaji kitu gani kingine, ndio maana wanaitwa wasimamizi na waangalizi wa ligi na wakishaitwa hivyo utajua ina maanisha nini."
 

TPLB ina majukumu gani?

Kasongo anasema watu wanatakiwa kujua TFF ndiyo imepewa jukumu la kusimamia soka hapa nchini na linapotokea tatizo lolote wao ndio wanakua watu wa kwanza kutazamwa.

"Ukiangalia TFF kazi yake kubwa ni kusimamia mpira wa miguu ambayo ameikasimisha kwa TPLB, hivyo unaweza kuona kwanini watu wana mapenzi makubwa na TPLB sababu ndio anasimamia na kuendesha shughuli yenyewe ya kuanzishwa TFF," anasema Kasongo.

Lakini ili iweze kuendesha lazima iwe na fedha kwa hiyo kazi nyingine ni kutafuta wadhamini, kuzitangaza ligi hizo, kutafuta mahusiano na ligi nyingine kubwa duniani, kutengeneza kanuni za kudhibiti matumizi ya fedha na mambo mengine mengi.
 

Mchakato unakwama wapi?

Kasongo anasema hii ni safari lakini anaamini ipo siku itakuwa huru kama ambavyo kila mmoja anapenda kuona ikifanya kazi yake na kuijisimamia.

"Acha tutengeneze mazingira ya kufika huko sababu mchakato siku zote huchukua muda mrefu na ipo siku tutafika huko ambako tunatarajia," anasema.

Angetile anasema kikwazo kikuu ni siasa za soka ukihusisha na siasa za nchi. Kiongozi wa mpira anakuwa na nguvu zaidi kama anaweza kuwa na mamlaka yote kwenye Ligi Kuu.

Wengi wanaona kujihusisha na maendeleo ya soka kwa ujumla, kama timu za taifa, mafunzo na mashindano ya vijana huwezi kuwa na nguvu.

"Labda tu pale timu za taifa zinapofanya vizuri kwa kuwa ndio wakati hata wanasiasa huziita kwa ajili ya kuipongeza, Kuitwa ikulu, bungeni na kwingineko. Wapo pia wanasiasa ambao wanataka kujitangaza kupitia soka.
 

TPLB ifanye nini ili iwe huru?

Kasongo anasema kwanza hawezi kuzuia watu kuzungumza kile wanachokiwaza kama iko huru au sio huru lakini suala ni muda na mchakato ambao utafika mwisho muda sio mrefu.

Angetile anasema kwa hali ilivyo sasa TPLB haiwezi kufanya lolote iwe huru kwa kuwa imetokana na TFF. Walioajiriwa na TFF hawawezi kujiondoa kwa mwajiri wao.

"Ili TPLB iwe huru lazima klabu ziamke na kudai chombo chao, chombo ambacho kitawajibika kwao na si kwa viongozi wa TFF, chombo ambacho kitajikita katika kuhakikisha ligi inaongezeka ubora na klabu zinastawi kifedha.

"Chombo ambacho kitahakikisha kunakuwa na haki sawa kwa klabu zote na si baadhi kupewa uzito kuliko nyingine, chombo ambacho kinaweza kuzuia wachezaji kwenda kutumikia timu zao za taifa wakati ambao si wa mechi za tarehe za Fifa hii hufanyika.

"Kulinda wachezaji nyota ambao ndio huvuta mashabiki na hivyo wadhamini kuweka fedha, chombo ambacho hakitakuwa kinasimamisha ligi hovyo kwa maslahi ya wachache, chombo ambacho kinaweza kushirikiana na idara za serikali kuweka viwango vya wachezaji wanaotakiwa wapewe ruhusa ya kufanya kazi (kucheza soka) nchini na si yeyote kama ilivyo sasa.

Hii haitawezekana kama klabu zitaenda kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi zikiwa na ajenda hiyo ya kuchagua watu watakaoongoza kuifanya TPLB iwe huru.