Hawa hapa wanaitosha Simba

Muktasari:

WINGA wa zamani wa Simba, Mnenge Suluja ameiuma sikio timu hiyo akiishauri kuwa makini kwenye dirisha la usajili na mipango ya kuboresha kikosi chao akiutaka uongozi kusajili wachezaji watano tu.

WINGA wa zamani wa Simba, Mnenge Suluja ameiuma sikio timu hiyo akiishauri kuwa makini kwenye dirisha la usajili na mipango ya kuboresha kikosi chao akiutaka uongozi kusajili wachezaji watano tu.

Tayari Simba imetangaza kumalizana na mshambuliaji, Moses Phiri raia wa Zambia atakayeongeza nguvu safu ya ushambuliaji ambayo haikuwa na makali msimu huu, huku ikitajwa pia kuwa kwenye mipango ya kumnasa kiungo Mnaigeria, Victor Akpan anayekipiga Coastal Union.

Suluja aliliambia Mwanaspoti kwa wachezaji wa ndani (wazawa) waliopo, hakuna haja ya kuongeza wengine kwani wengi wanalingana viwango na wataletwa na kushindwa kuisaidia timu huku wakiishia kutolewa kwa mkopo mwisho wa msimu.

Winga huyo alisema upande wa wazawa inapaswa kubaki ilivyo na nguvu ielekezwe kwa wachezaji wa kigeni watano wenye uzoefu watakaoziba mapungufu yaliyopo sasa ambao ni washambuliaji wawili, mabeki wawili wa kati na kiungo mmoja mshambuliaji.

“Wachezaji watano tu wanatosha kuiboresha timu msimu ujao, wasifanye usajili mwingi wa kuivuruga timu. Viongozi wawe makini kwa sababu msimu ujao utakuwa na ushindani zaidi.”

Kuhusu wachezaji wazawa alisema;

“Rai yangu wachezaji wa wazawa waongeze umakini, juhudi binafsi na mazoezi ya ziada kushindania namba kuliko kubweteka kila siku namba zinachukuliwa na wageni na kushindwa kuzisaidia timu zao.”

Alisema Simba ina faida ya kuwa na wachezaji wengi vijana waliobeba matumaini ya kikosi hicho akiwemo Jimyson Mwanuke, Peter Banda, Pape Sakho, Sadio Kanoute na Kibu Denis huku akiwataka viongozi kuwabakiza washambuliaji John Bocco na Chris Mugalu.

“Wachezaji wa ndani waliopo naona wanatosha hakuna haja ya kuleta wapya. Tunao wachezaji vijana wasiachwe wawape nafasi, mfano Mwanuke asitolewe kwa mkopo, nafikiri Bocco na Mugalu waendelee kuwepo na Bocco awe sehemu ya hamasa ya kikosi,” alisema Suluja.