Hili hapa picha zima Yanga kwa Mshery

ALIYEKUWA kipa wa Mtibwa Sugar, Aboutwalib Mshery sasa rasmi ni mali ya Yanga baada ya mabosi wa Jangwani kutumia jeuri ya pesa na umafia kumpata jana.

Mshery alisaini mkataba wa kuitumikia Yanga kwa miaka mitatu jana Jijini Dar es Salaam dakika chache baada ya kufika akitokea Tanga alikofuatwa na Yanga.

Mechi kati ya Mtibwa Sugar na Coastal Union iliyopigwa Jumanne na Mshery kuonesha kiwango bora zaidi akiisaidia timu yake kushinda bao 1-0 ugenini Tanga ndiyo ilikuwa ya Mwisho kwa kipa huyo kulidakia chama lake hilo la tangu utotoni.

Awali dili hilo liliingia ugumu baada ya viongozi wa Mtibwa kukataa kumuuza Msheri wakidai kuwa ni mchezaji tegemeo kikosini hapo hivyo hauzwi kwa gharama yeyote ile.

Baada ya hapo Msheri aliomba kuvunja mkataba kwani alikuwa tayari na mipango ya kujiunga Yanga na akawa tayari kutoa Sh 20 milioni kuvunja mkataba wa mwaka mmoja na nusu uliokuwa umebaki ndipo vigogo wa Mtibwa wakastuka na kuwaita mabosi wa Yanga mezani wakazungumza na kukubali kuwauzia kipa huyo.

Mjumbe wa kamati ya usajili ya Yanga mhandisi Hersi Said kupitia ukurasa wake wa Instagram ameweka wazi mbinu za kimafia alizotumia hadi kumpata Mshery na kusaini mkataba Yanga.

"Kwa mahitaji ya kipa kwa sasa katika klabu yetu ya Yanga na hali ya mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha ya klabu yake ya zamani (Mtibwa), haikuwa rahisi kumpata kipa huyu.

Jitihada kubwa zilifanyika kwa ushirikiano na manager wake George Job na hatimaye mwanga ukaonekana.

Akiwa na mchezo wa mwisho kwenye rangi za Mtibwa pale mkwakwani dhidi ya wagosi wa kaya, nikaanda usafiri wa kumleta Dar es salaam usiku ule ule," aliandika Hersi na kuongeza;

"Saleh Kiraka alikuwa nyuma ya usukani (Dereva) kumleta Dar es Salaam.

Akiwa anamsubiri waanze safari usiku ule, Mshery akaomba kuswali swala la I’SHAA ( sala ya saa mbili usiku ) tena aiswali JAMAA ( pamoja na waislam mskitini )

Salehe akamsubiri kwa madakika kadhaa na hatimaye akachoka, akanipigia simu na kuniuliza swali hili….

“Hivi Injinia mmemsajili kipa au imamuu wa Msikiti, mbona hatoki huko msikitini?,".

Baada ya hapo Msheri alitua Dar usiku ule na kusaini mkataba wa miaka mitatu Yanga na huenda akaanza kwenye mechi ya kesho dhidi ya Dodoma Jiji kwani jana alifanya mazoezi na Yanga pia kipa Djigui Diarra hayupo nchini alisafiri kuelekea kwao kujiunga na timu ya taifa la Mali inayojiandaa na fainali za mataifa ya Africa zitakazoanza mwezi ujao nchini Cameroon.