Hispania yaifuata Ureno fainali ikiifunga Ufaransa
Muktasari:
- Mchezo huo umeweka rekodi ya kuwa na mabao mengi zaidi katika historia ya UEFA Nations League.
Stuttgart, Ujerumani. Hispania imefuzu katika fainali ya UEFA Nations League baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-4 dhidi ya Ufaransa katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa jana kwenye Uwanja wa MHP Arena, Stuttgart, Ujerumani.
Katika mchezo huo ullioshuhudia jumla ya mabao tisa, kinda wa miaka 17, Lamine Yamal, aliibuka shujaa kwa kuifungia Hispania mabao mawili, na kusaidia timu yake kutinga fainali ya tatu mfululizo ya Nations League.
Hispania ilianza kwa kasi na kujipatia mabao mawili ya haraka kupitia kwa Nico Williams na Mikel Merino ambayo yalipatikana ndani ya dakika 25 za kwanza. Yamal aliongeza bao la tatu kwa penalti katika daikika ya 54 kisha dakika moja baadaye Pedri alifunga bao la nne kwa Hispania.
Ufaransa ilijibu mapigo kupitia kwa Kylian Mbappé aliefunga kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 59, kabla ya Rayan Cherki kufunga la pili wakati bao la tatu lilipatikana baada ya beki wa Hispania, Dani Vivian kujifunga katika dakika ya 54, kabla ya Randal Kolo Muani kufunga bao la nne kwa kichwa katika dakika za majeruhi.
Hata hivyo, juhudi za Ufaransa kurejea mchezoni hazikutosha, na Hispania ikasonga mbele kwa ushindi wa 5-4.
Lamine Yamal aliendelea kuonyesha ubora wake kwa kufunga mabao mawili katika mchezo huo, ambayo yamemfanya kuhusika kwenye mabao 48 katika mechi 57 msimu huu.
Kwa ushindi huo, Hispania sasa itakutana na Ureno katika fainali ya UEFA Nations League, mchezo unaotarajiwa kuwa wa kusisimua na kiushindani. Kwa upande mwingine, Ufaransa itakutana na Ujerumani katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu. Mchezo wa jana umeweka rekodi ya kuwa na mabao mengi zaidi katika historia ya UEFA Nations League