Hitimana afichua siri za Mkude

Saturday January 01 2022
hitimana pic
By Daudi Elibahati

ALIYEKUWA kocha msaidizi wa Simba, Thierry Hitimana ameeleza namna alivyomsaidia kiungo wa timu hiyo Jonas Mkude kurejea kwenye makali.

Mkude anayetajwa kuwa kipenzi cha mashabiki wa klabu hiyo, alikuwa kwenye wakati mgumu kupata nafasi chini ya Kocha aliyetimuliwa klabuni hapo, Didier Gomes, ambaye alipenda kumtumia zaidi Mganda, Taddeo Lwanga kabla ya kupata jeraha la goti.

“Niliongea naye kwa muda mrefu na nilichokuwa namwambia atambue kuwa soka ni kazi ya muda mfupi, hivyo awekeze nguvu ndani ya uwanja,” alisema Hitimana na kuongeza:

“Alibadili fikra zake na akaanza kujituma na matunda yake yanaonekana, jambo ambalo najivunia kwake kumuona akifanikiwa.”

Kuonyesha kuwa kiungo huyo anazidi kuimarika aliweza kutoa pasi ya bao (asisti) aliyofunga beki wa kushoto wa timu hiyo Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwenye mchezo wao dhidi ya KMC waliifunga mabao 4-1 kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Ijumaa iliyopita.

Uongozi wa Simba uliachana na kocha huyo kutoka Rwanda baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja kandarasi baina ya pande mbili.

Advertisement

Hitimana alijiunga na Simba Septemba 11 kama kocha msaidizi kabla ya kumkaimisha ukocha Mkuu baada ya kumtema Didier Gomes, Oktoba 26.

Gomes aliyefutwa kazi baada ya kushindwa kuivusha timu hiyo kuingia hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha huyo mwenye uzoefu na soka la Tanzania amewahi kufundisha, Namungo aliyoachana nayo mwaka 2020 kisha kutua kwa muda Mtibwa Sugar, kabla ya kuchukuliwa na Simba.

Hitimana aliwahi pia kuwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Rwanda ya (U-23) mwaka 2012, kisha kuinoa Rayon Sports kabla ya kuiongoza Bugesera FC zote za nchini kwake.

Advertisement