Hitimana Thiery ang’atuka Mtibwa Sugar

Muktasari:

Kwa sasa Kocha huyo yupo nchini kwao Rwanda, ambapo kabla ya kujiunga na Mtibwa Sugar aliitumikia Namungo aliyoipandisha daraja na kuipeleka kombe la shirikisho Afrika.

Mwanza. Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Hitimana Thiery amesema hatarajii kurudi nchini kuendelea na majukumu yake klabuni humo kutokana na vitendo alivyofanyiwa kwenye benchi la ufundi ikiwamo kuingiliwa majukumu.

Thiery ameliambia Mwanaspoti Online kuwa licha ya kuvumilia kwa muda mrefu lakini amefikia maamuzi hayo ili kulinda heshima yake na timu hiyo ambayo inapambana kukwepa kushuka daraja.

Alisema licha ya taarifa zake kuwasilisha kwa mabosi mara kadhaa, lakini viongozi wamekuwa wagumu kufanya maamuzi, hivyo ili kuepuka lawama ameamua ajiweke kando na kwamba kwa sasa ameamua kupumzika hadi msimu ujao.

“Nilishawasilisha malalamiko kwa uongozi kuhusu kuingiliwa majukumu yangu na walio chini yangu, lakini hakuna hatua yoyote, kwahiyo nimeamua niwaachie timu, kama haitoshi sikuwa na mkataba” amesema Thiery.

Hata hivyo Katibu Mkuu wa Mtibwa Sugar, Majidi Bakari amesema bado wanafahamu kocha huyo ni mali yao na kwamba wanaamini hata mechi yao ya Ijumaa dhidi ya Azam atakuwapo.

Taarifa zaidi endelea kufuatilia Mwanaspoti