Huyu ndiye Ancelotti anayesubiri rekodi nyingine

Muktasari:

  • Jumamosi ya wiki ijayo kikosi cha Madrid kitakuwa kwenye Uwanja wa Wembley kuvaana na Borrusia Dortmund kwenye mchezo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote kutokana na umaarufu wa michuano hiyo.

Madrid, Hispania. Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti anakwenda kwenye mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki ijayo akiwa anatafuta rekodi nyingine kwenye michuano hiyo mikubwa Ulaya.

 Jumamosi ya wiki ijayo kikosi cha Madrid kitakuwa kwenye Uwanja wa Wembley kuvaana na Borrusia Dortmund kwenye mchezo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote kutokana na umaarufu wa michuano hiyo.

Ancelotti  ambaye anatajwa kuwa kocha mkongwe kwa sasa kwenye michuano hiyo anapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo ambao utakuwa wa 15 kwa Real Madrid ambayo imekuwa ikifanya vizuri zaidi kwenye  michuano hiyo kwa kipindi kirefu sasa.

Kocha huyo mwenye miaka 64, akiwa ameshafundisha timu saba kubwa barani Ulaya hadi sasa ndiye kocha mwenye makombe mengi zaidi ya Ulaya akiwa nayo manne.

Mbali na rekodi za Uefa, lakini pia anashikilia rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutwaa ubingwa wa ligi kwenye nchi nne kubwa za Ujerumani, Italia, Ufaransa na England.

Kocha huyo wa zamani wa Chelsea amekuwa anatajwa kuwa anaweza kustaafu baada ya mchezo huu ingawa ni jambo ambalo halijawekwa wazi.


Kocha wa michezo 200

Ancelotti kwa sasa anashikilia rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kufundisha michezo 200 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kocha huyo aliweka rekodi hiyo wakati wa mchezo wa robo fainali dhidi ya Manchester City msimu wa 2023/24.

Idadi hiyo ya michezo ameiweka akiwa na klabu za AC Milan, Chelsea, Bayern, Juventus, Paris, Parma, Real Madrid na Napoli. Idadi hiyo ya klabu inamfanya kuwa kocha mwenye uzoefu mkubwa zaidi kwenye michuano hii kama kocha na mchezaji akiungana na Frank Rijkaard, Zinédine Zidane na Pep Guardiola.

Mafanikio ya kombe hili ameyapata akiwa na AC Milan alipotwaa ubingwa msimu wa 2003, 2007, lakini akatua Madrid napo na kuchukua ubingwa misimu ya 2014, 2022 na sasa anatafuta ubingwa huo kwa mara ya tatu na timu hiyo.


Kocha aliyeshinda michezo mingi:

Baada ya kufundisha michezo 200 na zaidi kwenye michuano hiyo ya Uefa, Carlo anashikilia rekodi nyingine ya kuwa kocha aliyeshinda michezo mingi zaidi kwenye michuano hiyo mikubwa.

Kocha huyo ameshinda michezo 115, akiwa mbele ya magwji wakubwa, Alex Ferguson na Arsene Wenger ambao hawapo kwenye soka kwa sasa, kwenye ushindani wa makocha ambao bado wanafundisha anaweza kufikiwa na Pep Guardiola ambaye ameshinda michezo 109 kati ya 169 ambayo ameshafundisha, mwingine aliyekaribu ni Jose Mourinho aliyeshinda 77 kati ya 169.


Michezo ya jumla:

Kocha huyo mwenye uzoefu wa hali ya juu anashikilia rekodi ya jumla ya kufundisha michezo 1,341, kuanzia ameanza kazi hiyo akiwa ameshinda 794 ametoka sare 301 na kupoteza 246, kwenye maisha yake yote ya kufundisha soka. Katika Uefa Ancelotti amefika fainali mara sita na kutwaa ubingwa mara nne ikiwa ni mara mbili tu amekosa ubingwa huo baada ya kufika fainali.