Ishu ya Al Hilal ya Sudan kucheza Ligi Kuu Bara iko hivi

Muktasari:

  • Baada ya maswali mengi ya wadau wa michezo kuhusu Al Hilal ya Sudan kucheza Ligi Kuu Bara TFF imeweka wazi kila kitu wazi huku ikiwataja hadi waamuzi.

Dar es Salaam. Klabu ya Al Hilal ya Sudan itashiriki Ligi Kuu ya Bara msimu ujao lakini kwa vigezo maalumu, Mwananchi limeambiwa.

Si klabu hiyo tu, hadi waamuzi wa soka wa Sudan walioko Tanzania watachezesha Ligi msimu ujao kutokana na machafuko yanayoendelea nchini kwao yaliyosababisha michezo kusimama kwa muda usiojulikana.

Mwananchi linajua Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), imeshakutana na kulipitisha suala hilo tayari kwa msimu ujao, hivyo mashabiki wajiandae kumuona kocha wa viwango Florent Ibenge na chama lake kwenye viwanja vya Ligi Kuu Bara.

Ibenge ni kocha mkubwa Afrika akiwa na ubingwa Kombe la Shirikisho Afrika, msimu wa 2021/2022 akiwa na RS Berkane.

Cliford Mario Ndimbo, ambaye ni Ofisa Habari wa TFF, amelithibitishia kwamba Hilal itacheza kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao lakini kwa vigezo maalumu lengo likiwa kuongeza ushindani na kuitangaza ligi yetu.

"Ni kweli Hilal wameomba kushiriki ligi yetu na suala lao limeshajadiliwa na kupitishwa na Kamati ya Utendaji, kwa hiyo msimu ujao watacheza mechi zote za Ligi kama timu nyingine yoyote ya Tanzania," alisema Ndimbo.

"Tofauti yao na timu nyingine ni kwamba pointi zao hazitahesabiwa, watashiriki kama mechi za kirafiki wala kwenye msimamo hawatasomeka, TFF imewakubalia ombi lao kwavile litakuwa na faida kubwa kwenye ligi yetu.

"Hilal ni timu kubwa wataitangaza ligi yetu, watatoa ushindani wa kweli kwa timu zetu, hata mapato yataongezeka kwa klabu zetu kwavile itapata nafasi ya kucheza na timu zote tofauti na awali ambapo ilicheza dhidi ya timu za Dar es Salaam tu," aliongeza Ndimbo.

Mbali na timu hiyo, pia TFF imewapitisha waamuzi wote wa Sudan walioko Tanzania kuchezesha Ligi msimu ujao kama sehemu kuongeza ubora kwavile kwasasa wamekuwa tu nchini wakifanya mazoezi.

Uamuzi huo wa TFF, huenda ni wa kwanza wa aina yake hapa nchini katika miaka ya hivi karibuni kwa timu ngeni kucheza Ligi ya nchi nyingine ili kujiweka fiti bila kupata chochote.

Ikumbukwe Hilal ilishindwa kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa katika dakika za mwisho msimu huu na tayari imetuma ofa kwa klabu ya Azam ikitaka kumsajili straika wao, Prince Dube kama ilivyo kwa Simba.