Joyce Lema: Kiungo wa Fountain Gate anayemzimia Feitoto

Mmoja kati ya wachezaji wanaofanya vizuri katika ligi Kuu ya Wanawake (WPL) kwa sasa  ni kiungo wa Fountain Gate Princess na timu ya Taifa ya vijana ya wanawake (U-17) ‘Serengeti Girls’, Joyce Lema.
Joyce amekuwa na kiwango bora si msimu huu pekee, bali hata msimu uliopita, aliisaidia timu yake kushika nafasi ya pili kwenye WPL  iliyomalizika kwa Simba Queens kutwaa ubingwa.
Kiungo huyo, ambaye humudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji na mchezeshaji alikuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji wa Serengeti Girls waliocheza katika  mashindano ya Kombe la Dunia kwa vijana, mwaka jana, nchini India.


SAFARI YA INDIA
Kiungo huyo anasema hatasahau alipopata nafasi ya kuliwakilisha Taifa katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa vijana nchini India akiwa na Serengeti Girls.
Anasema kupitia mashindano hayo amejifunza vitu vingi ambavyo vinamsaidia hadi sasa katika uchezaji wake.
“Nilichojifunza wenzetu wamepiga hatua kubwa mno na natakiwa kuzidi kujituma ila niseme ninafuraha na ile imekuwa historia kubwa katika masiha yangu.
“Nimepata cha kukiambia kizazi changu kwamba na mimi nilicheza Kombe la Dunia, ila bado naendelea kupambana kuhakikisha nazidi kufanikiwa,” anasema kiungo huyo mrefu kwa umbo.


HATAISAU MCHEZO NA JAPAN
Kabla ya mashindano hayo, timu hiyo iliweka kambi ya wiki mbili katika Mji wa Southompton, nchini England, kwa ajili ya maandalizi.
Anasema kambi hiyo iliwapa hali ya kuajimini na kujiona wanaweza kucheza na timu yoyote kwani walifanya mazoezi ya kutosha pamoja na kucheza michezo ya kirafiki.
Joyce anasema walikuwa na matarajio makubwa ya kufanya vizuri, lakini katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Japan walikubali kichapo cha mabao 4-0.
“Mchezo ule kila nikikumbuka hadi leo naumia kwa sababu nilikuwa nimeupania sana, lakini matokeo yakawa vile,” anasema.

HUMWAMBII KITU KWA FEISAL
Kama kuna mchezaji ambaye Joyce anamhusudu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ya wanaume basi ni Feisal Salum ‘Feitoto’ wa Yanga.
“Raha sana kumwangalia jinsi anavyocheza, kuna vitu najifunza kutoka kwake kwa jinsi anavyocheza.
Anasema pia anapenda uchezaji wa kiungo wa Singida Big Stars, Yusuphu Kagoma.
“Kwa upande wa wanawake napenda sana uchezaji wa Amina Bilal wa Yanga Princess, amekamilika, anajua uwanjani anafanya nini,” anasema kiungo huyo mwenye ndoto ya kucheza soka nchini Sweden.


ATAKA FURSA ZAIDI
“Hili kwenu wazazi, acheni kuwaona watoto wa kiume pekee ndiyo wanajua soka, hata sisi tunaweza tena sana, bahati mbaya kwetu hatuonekani kama ni watu sahihi wa mchezo huu.
“Ombi langu, mpira wa miguu si wa wanaume pekee, nimefika nchi nyingi sababu ya soka, naendelea kuliheshimu nikiwaambia wazazi kuhusu haya wawe wananielewa,” anasema nyota huyo akitoa ushauri kwa wazazi.


KAKA ALIGUNDUA KIPAJI
Kipaji cha Joyce kiligunduliwa na kaka yake, ambaye anamtaja kwa jina moja la Rajabu, ambaye alikuwa akimtaka kila siku kuendelea kucheza bila kukata tamaa.
“Mwanzo hata mimi nilikuwa kama sijiamini, lakini kila siku kaka yangu huyo alikuwa akinisisitizia, namshukuru sasa hivi nimekuwa mchezaji mkubwa na nachezea timu ya Taifa,” anasema Joyce.


ALIWAHI KUZINGUA
Anasema 2017, wakati huo akiichezea timu ya Fair Play walikuwa na mechi dhidi ya JKT kwenye Uwanja wa Karume, Dar es salaam.
“Nilianzia benchi, zikiwa zimebaki dakika nane, kocha wetu  akaniambia nikapashe ili niingie, nikagoma, kwanini ananiingiza mechi bado dakika nane.
“Kocha alikasirika sana na kama mechi nne hivi akawa ananiweka benchi tena jukwaani, ila kuna kiongozi alinifuata akaniambia nilimkosea sana kocha, nikamuombe radhi.
“Kweli, nilikwenda kumuomba radhi, mechi iliyofuata akanipa nafasi ya kucheza kwa dakika 90, ni tukio ambalo nalikumbuka sana kwa sababu nilifanya utoto,” anasema.  


ATABIRI UGUMU
Anasema ameiangalia ligi ya msimu huu na kutabiri kutakuwa na ugumu kujua nani atatwaa ubingwa.
“JKT wapo vizuri, Simba Queens, Yanga Queens wapo vizuri  na sisi pia tupo vizuri, huwezi kutabiri nani anakuwa bingwa,” anasema kiungo huyo.
Joyce amezaliwa katika hospitali ya Mount Meru, jijini Arusha, amesoma shule ya msingi Kimandolu na sekondari ya Kimaseki za jijini humo, amewahi kuichezea timu ya The Tiger ya Arusha.