Jude Bellingam kinara wachezaji wenye thamani kubwa duniani
LONDON, ENGLAND. Taasisi ya uchunguzi ya CIES Football Observatory imetoa orodha ya wachezaji 100 wenye thamani kubwa zaidi duniani kwa sasa, huku staa wa Real Madrid, Jude Bellingam akiwa namba moja.
Inaelezwa CIES imetoa orodha hiyo kwa kuzingatia vigezo mbalimbali kama sifa za klabu ambazo wachezaji wanachezea, muda wa mkataba, ada za awali, kiwango cha mchezaji, sifa za mchezaji na umaarufu wake.
Jude anaongoza katika orodha hiyo akiwa ndiye mchezaji wa mpira wa miguu mwenye thamani kubwa zaidi kwa mwaka 2024 hadi sasa thamani yake ikiwa Euro milioni 251.
Mbali na Bellingham, nafasi ya pili inashikiliwa na Erling Haaland kutoka Manchester City mwenye thamani ya Euro milioni 221, kisha Vinicius Jr wa Real Madrid anamaliza nafasi tatu za juu kwa thamani ya Euro milioni 205.
Mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kwenye orodha hiyo ambaye ameshika nafasi ya nne ni Lamine Yamal anayekadiriwa kuwa na thamani ya Euro milioni 180, ikiwa ni baada ya kung'ara mwaka 2024 akiisaidia Hispania kuchukua ubingwa wa Euro.
Kylian Mbappe, amewekwa nafasi ya tano akiwa na thamani ya Euro milioni 175. Wachezaji wengine waliopo humo ni Bukayo Saka anayeshika nafasi ya sita akiwa na thamani ya Euro milioni 157 milioni, Florian Wirtz kutoka Bayer Leverkusen mwenye thamani ya Euro milioni 151 anashika nafasi ya saba.
Cole Palmer nafasi ya nane kwa Euro milioni 150, Phil Foden wa tisa kwa Euro milioni 144 wakati Rordygo Goes akifunga kumi bora akiwa na thamani ya Euro milioni 141.