Kagera Sugar vs Geita Gold kuendelea leo

Mchezo namba 21 wa Ligi Kuu Bara kati ya Kagera Sugar dhidi ya Geita Gold FC ambao uliahirishwa kwasababu ya hitilafu ya taa uwanjani utachezwa  leo saa 10 jioni kwa kumaliziwa dakika 51 zilizosalia kulingana na kanuni ya ligi Kuu kifungu cha 34:3 kuhusu kuahirishwa kwa mchezo.

"Mchezo ulioahirishwa kwa kifungu 34:1.4 utachezwa siku inayofuata  au muda mwingine wa karibu zaidi kadiri ratiba inavyoruhusu",

Mchezo huo utachezwa kwa vipindi viwili kwa kumalizia dakika sita kukamilisha  kipindi cha kwanza na kipindi cha pili dakika 45.

Mchezo huo uliahirishwa jana baada ya kuchezwa dakika 39 tu na kisha taa za uwanjani kuzima na hivyo kuhairishwa.

Hadi kuahirishwa kwa mchezo hakuna timu yeyote iliyoweza kupata bao.

Uongozi wa Kagera umesema mchezo utakuwa bure kwa mashabiki waliotoa viingilio vyao jana na wale ambao hawakutoa wataruhusiwa kuingia kutazama mchezo