Kalenda ya Fifa yazibeba Simba, Yanga

Muktasari:

  • Yanga imepangwa kukutana na Mamelodi katika mechi za robo fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Simba ikipewa Al Ahly na timu hizo zimetoa wachezaji walioitwa timu za taifa, lakini kalenda hizo za FIFA na ratiba ya mechi za nyumbani zinawabeba zaidi Simba na Yanga, kuliko wapinzani wao watakaocheza ugenini mechi za kwanza.

Dar es Salaam. Uwepo wa mechi za kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ni kama imewarahisishia kazi Simba na Yanga katika maandalizi ya mechi za robo fainali kutokana na wapinzani wao Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Al Ahly ya Misri, kuachia asilimia kubwa ya mastaa wa kikosi cha kwanza kabla ya kuja kuvifuata vigogo hivyo.

Yanga imepangwa kukutana na Mamelodi katika mechi za robo fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Simba ikipewa Al Ahly na timu hizo zimetoa wachezaji walioitwa timu za taifa, lakini kalenda hizo za FIFA na ratiba ya mechi za nyumbani zinawabeba zaidi Simba na Yanga, kuliko wapinzani wao watakaocheza ugenini mechi za kwanza.

Muda mchache baada ya droo, Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andrew Ntime alisema haoni kama ni vyema wachezaji wa timu hiyo kwenye na kikosi cha Stars.

"Nafikiri siyo sawa, ilikuwa vyema kama wangebaki kuendelea na mazoezini ya pamoja.

Ipo hivi. Wakati  wachezaji watano wa Yanga wameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, ambao ni Abuutwalib Mshery, Ibrahim Hamad Bacca, Bakary Mwamnyeto, Mudathir Yahaya na Clement Mzize ni watatu tu wana uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza.

Kati ya wachezaji hawa ambao wamekuwa wakianza kwenye kikosi cha Yanga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni Bacca, Mwamnyeto na Mudathir jambo ambalo ni ahueni kwao.

Kwa upande wa wapinzani wao Mamelodi, wachezaji 10 wameitwa kwenye kikosi cha Afrika Kusini, Bafana Bafana, ili kujiandaa na mechi za kimataifa za kirafiki.

Wachezaji walioitwa Bafana Bafana ni; Ronwen Williams, Grant Kekana, Terrence Mashego, Aubrey Modiba, Mothobi Mvala, Khuliso Mudau, Themba Zwane, Teboho Mokoena, Thapelo Maseko na Thapelo Morena wote wakiwa wanacheza kikosi cha kwanza cha Mamelodi na wote walikuwepo kwenye kikosi cha Afcon 2023.

Bafana Bafana itacheza michezo miwili ya kirafiki, mmoja nyumbani dhidi ya Andorra, Ijumaa ya Machi 22, huku mwingine ukiwa ugenini dhidi ya Algeria, Machi 27, baada ya hapo watajiandaa na safari ya kuja Dar ambapo watacheza na Yanga, Machi 29 kwa Mkapa.

Pamoja na kwamba Namibia haijafahamika itacheza na nani, pia Mamelodi wanaweza kumruhusu Peter Shalulile ambaye ni nahodha wa nchi hiyo, hivyo wachezaji wake watakaoondoka watafikia 11 tofauti na idadi ile ya Yanga.

Hata hivyo, kocha wa Yanga Miguel Gamondi, anaweza kuwa na muda wa angalau siku mbili kukaa na mastaa wake kwa kuwa Stars inacheza mchezo wa mwisho Machi 25 dhidi ya Mongolia Barani Ulaya na inaelezwa kuwa siku hiyohiyo wataanza safari ya kurejea nchini.

Asilimia kubwa ya wachezaji wa Yanga wapo kwenye kikosi cha Taifa Stars ambacho kina michezo miwili kama ilivyo kwa Afrika Kusini, lakini ahueni iliyopo ni itacheza mapema zaidi dhidi ya Bulgaria Machi 22 na Mongolia, Machi 25.

Wachezaji ambao wanaweza kuchelewa kurejea kambini kwa Yanga ni Djigui Diarra ambaye taifa lake, Mali litacheza dhidi ya Mauritania, Machi 22 na dhidi ya Nigeria Machi 26 na Stephane Aziz Ki ambaye Burkinafso itacheza dhidi ya Libya, Machi 22 na dhidi ya Niger, Machi 26 wakiongoza wachezaji wanaoanza kikosi cha kwanza hadi kufikia watano.

Wakati mambo yakiwa hivyo kwa Yanga, upande wa wapinzani wa Simba, Al Ahly yenye wachezaji 11 timu ya Taifa ya Misri ambao ni Oufa Shobeir, Mohamed Abdelmonem, Rami Rabia, Mohamed Shokry, Mohamed Hany, Akram Tawfik, Marwan Ateya, Ahmed Kouka, Emam Ashour, Afsha Afsha na Hussein El Shahat watasafiri kwenda New Zealand kwa ajili ya mchezo mmoja wa kirafiki unaotarajiwa kuchezwa, Machi 22.

Hili linaweza kuwa tatizo kwa Simba kwa kuwa hawa watakuwa na zaidi ya siku tano za maandalizi kambini kwao, kwani wana mchezo mmoja tu. Mchezaji pekee ambaye anaweza kuchelewa kurejea kwa Mafarao hao ni Percy Tau tu ambaye anaichezea Bafana Bafana na ainfanya Ahly ifikishe mastaa 12.

Nyota wa Simba ambao ni sehemu ya kikosi cha Taifa Stars ni Aishi Manula, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Kennedy Juma na Kibu Denis, Saido Ntibazonkiza Burundi huku kukiwa na uwezekano wa Clatous Chama kutojiunga na Zambia kwa kuwa mchezo wao dhidi ya Eritrea umefuatwa.

Kati ya mastaa hao Simba itawakosa wachezaji wawili tu wa kikosi cha kwanza ambao ni Tshabalala na Saido.

Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha anaonekana kuwa na idadi kubwa ya mastaa wake, kambini akiwemo Che Malone Fondoh, Freddy Kouablan, Inonga, Ayoub Lakred, Shomary Kapombe, Fabrice Ngoma, Babacar Sarr na Pa Jobe ambao hawajaitwa timu zao za taifa.

Hii ina maana kuwa Simba itakuwa na nafasi kubwa zaidi na mastaa wake wa kikosi cha kwanza kuendelea na mazoezini.

Saido Ntibazonkiza anaweza kurejea pamoja na wachezaji wa Taifa Stars kwa kuwa Burundi inacheza mchezo wa pili nyumbani dhidi ya Botswana, Machi 25. Henock Inonga Baka alipata majeraha kwenye mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Singida FG hivyo anaweza kusalia kambini kwa maandalizi ya kuivaa Al Ahly.

Hata hivyo jana ilielezwa kuwa timu za Simba na Yanga zinataka kuomba wachezaji wake wabaki ambapo Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo alisema hawajapata barua yoyote.

"Wanafahamu njia ya kupitia, TFF hadi sasa haijapata barua yoyote kutoka kwenye hizo timu, lakini ratiba hii ya mechi ilikuwa inafahamika muda mrefu," alisema Ndimbo.


WASIKIE WADAU

Kwa upande wa kocha wa zamani wa Yanga Boniface Mkwasa, alisema ni vyema shirikisho la soka liangalie pia ratiba ya klabu na kuzisaidia pia.

"Ni vyema TFF kwa kuwa ndiyo baba wa soka nchini, wakaangalia na ratiba ya klabu kwa kuwa wanifahamu zinakabiliwa na michezo migumu hapo mbele, lakini pia michezo kama hii siyo lazima wachezaji wa Simba na Yanga waitwe ilikuwa nafasi ya makocha kuwapa nafasi vijana na hawa wengine wangejiandaa vizuri na michezo yao alisema Mkwasa kocha wa zamani wa Taifa Stars na Yanga.

Kocha wa makipa, wa zamani wa Singida FG Peter Manyika  alisema "Kama ni wachezaji wanaoanza kikosi cha kwanza, wanakuwa wamezoeana, hivyo hakuwezi kuwa na tofauti yoyote, labda cha kuhofia ni endapo wakipata majeraha, inakuwa inampa changamoto kocha kubadili mipango yake."

Kocha upande wa Mussa Hassan Mgosi ambaye kwa sasa anaifundisha Simba Queens, yeye alisema "Faida ya mchezaji akiitwa timu ya taifa kama atakuwa amecheza basi atarejea kiwango chake kikiwa kizuri cha kuisaidia timu yake, ila changamoto inakuja ikipata majeraha ama kama hakucheza itabidi kufanya mazoezi ya kujiweka sawa, nafikiri hapa ndiyo kuna tatizo, lakini kuitwa siyo shida hata kidogo."