Kaseba: Mlokole anayeasa wanamichezo

Dar es Salaam. Bondia mkongwe wa ngumi na mateke 'Kick boxing', Japhet Kaseba (44), anatoa somo la maisha kwa wanamichezo kuandaa maisha yao nje na kazi hiyo ili kuepukana na msongo wa mawazo baada ya kustaafu.

Kaseba anasema kuna umri ambao utamfanya mchezaji awe nje ya kazi, hivyo chochote wanachokipata kwa sasa wakiwa kazini wasiache kuyakumbuka maisha yao ya baadaye.

"Ulaya mchezaji ama bondia anapostafu anakuwa bado yupo kwenye piki ambayo mashabiki wanatamani kumuna ila sisi lazima uzomewe na mashabiki ndipo ung'atuke hilo linatokana na kukosa maandalizi.

"Ninachoshauri wakati wakifanya starehe kutokana na ustaa wao, wakumbuke kuna maisha halisi yanawasubiri, binafsi nimestafu nikiwa na umri mdogo na sasa nacheza kama burudani kuwapa raha mashabiki wangu na sio mapambano ya ubingwa."


Alama alizoacha

Anasema kipindi anapigana ngumi za mateke zilikuwa juu, alifanikiwa kubeba mikanda mikubwa miwili duniani, wa World Kick Boxing League (WKL) na World Kick boxing Circuit (WKC).

"Mikanda ambayo ilinisaidia kuwavutia mashabiki hadi viongozi wa Serikali, kwani kupitia ubingwa huo nilitangaza nchi, kwani nchi nilizokuwa nakwenda ilitajwa Tanzania na bendera yake ilikuwa inapepea;

"Aina yangu ya upiganaji wa kuwavunja miguu wapinzani wangu hasa wa kutoka Ulaya, India, Philippines na nchi nyingine nyingi duniani ulikuwa unawavutia mashabiki wangu kuja kunitazama nilipokuwa na pambano.

"Haikuwaishia hivyo, kuna nchi zilikuwa zinanialika kwenda kuwapandisha viwango mabondia wao kama Kenya, mmojawapo alikuwa Alphonce Kakaa na Uganda ni Golola Moses, nisingeweza kupewa fursa hiyo endapo ningekuwa nacheza chini ya kiwango," anasema.

Kaseba, mwasisi wa mchezo huo anasema kwa hapa Tanzania amewatengeneza Captain Kabongo na Pendo Njau na wengine ni Jesca Mfinanga, Feriche Mashauri, Boyka, Imani, Mohamed Alkaida, Kanda Kabongo, Emanuel Shija, Mrisho Dame na wengine wengi.


Alichokivuna

Anasema kupitia mchezo huo umemfanya afahamiane na watu wengi duniani, umempa heshima kubwa ndani na nje ya nchi ambapo akiwa na jambo lake ni rahisi kusaidiwa.

"Nje na kufahamiana na watu, nina kila kitu ambacho binadamu anatakiwa kumiliki, mfano nyumba na magari, natunza familia yangu na kusomesha watoto wangu, hivyo umenilipa, kikubwa zaidi nina afya njema;

"Siwezi kuweka kila kitu hadharani, lakini nina ujasiri wa kuwaambia vijana wanaotaka kuingia kwenye mchezo huo wasiogope, kwani unalipa endapo tu kama watamaanisha na kuzingatia miiko yake, wasirundikane kwenye soka," anasema.


Nusu apoteze maisha

"Tukio la kuzimia ulingoni baada ya kumaliza pambano langu la roundi 10 baada ya kumshinda Master Yusufu Mzaire, bingwa wa DR Congo, sitakuja kulisahau kwenye maisha yangu yote na lilisababisha nimrudie Mungu wangu.

"Huo kwangu ni ushuhuda mkubwa sana, nilijihisi kifo, kilichosababisha nilizoea kupigana raundi moja hadi tatu, lakini pambano lile lilikuwa la raundi 10, kwanza nilikuwa na mwili mnene hivyo upepo ulijaa kifuani," anasimulia.

Anasema tangu kipindi hicho akaamua kuokoka na anasali kanisa la Akuzamu na kwamba isingekuwa mchezo huo angekuwa mtumishi wa Mungu kwa kuhubiri injili.

"Ningekuwa mhubiri wa neno la Mungu kwani ndiyo kitu nilichokuwa nakipenda zaidi, huku kwenye ngumi niliingia kutafuta maisha, ila tukio la kuzimia likanirudisha rasmi kwa Mungu, maana maisha yetu ni mafupi sana," anasema.

Anasema kwenye michezo kuna wakati mwingine watu wanawekeana roho mbaya ili mladi tu kupigania vitu ambavyo kila mmoja ataviacha duniani na vinapita.

"Kila mtu ana kipaji chake ambacho Mungu amempatia, hakuna haja ya kuwekeana roho mbaya na si vyema kufurahia mateso ya mtu huo ni udhaifu," anasema mkali huyo wa ngumi za mateke.


Simba Queens

"Naifundisha mazoezi familia ya Mohammed Dewji 'Mo' kwa muda mrefu sana, ni kama ndugu sasa, hivyo Fatema, mdogo wake Mo ndiye aliniomba nikaisaidie Simba Queens kuifundisha mazoezi ya nguvu, ujasiri na nidhamu ya mazoezi zaidi.

"Kwa sasa siendi kulingana na umbali, kwenda na kurudi kwangu nilikuwa natumia muda mwingi na ratiba zangu zinakuwa zinanibana, kwani nafundisha na watu binafasi, lakini ikitokea wananihitaji nitawasaidia," anasema.

Anasema kupitia kuifundisha Simba Queens, amegundua namna mabinti walivyoamka na kupambana kuonyesha vipaji vyao ambavyo wakifanya bidii anaamini vitawalipa na maisha yao yatapiga hatua kiuchumi.


Anachokifanya kwa sasa

"Nilichaguliwa kuwa mwenyekiti wa mabondia wote wa mgumi za kulipwa Tanzania, pia nina gym yangu ambayo ninashirikiana na viongozi wenzangu kina Kanda Kabongo, Pendo Njau kuhakikisha tunanyanyua na kuviendeleza vipaji vipya ili vifikie au vizidi mafanikio yetu.

"Pia nafanya kazi zangu za kufundisha watu mazoezi binafsi kama kuwatengenezea ufiti, kupunguza uzito na mambo mengine mengi yanayohusu michezo," anasema.

Lakini kwa upande wa familia yake ya mke mmoja na watoto watano, anasema ni mmoja wa mwisho ndiye anafuata nyayo zake pia anapenda mpira wa miguu.

"Kijana wangu wa mwisho simshangai kwani na mimi nilikuwa napenda sana mpira, ingawa nilitoboa kwenye ngumi, nitamsapoti kwa kile anachokipenda na wengine waliobakia wanapenda sana kusoma, hivyo najitahidi kuwatimizia ndoto zao," anasema.

Amepigana ngumi zaidi ya miaka 10 na anasema alianza karate akiwa na miaka saba na kustaafu 2008, akiwa na miaka 28, baada ya kurejea Tanzania akitokea Japan ambako aliishi miaka miwili.

"Nimestafu nikiwa na umri wa kuendelea kucheza kwa sababu nilikuwa nakosa wapinzani, ndiyo maana meneja wangu alikuwa Mjapan alitaka niishi huko ila maisha yalikuwa juu na familia ilikuwa Tanzania, sikuona sababu ya kuendelea kukaa nchi hiyo.

"Ndani ya miaka miwili niliyoishi Japan nilikuwa nacheza mapambano mbalimbali ikiwemo ya dunia nzima, ambayo iliwakutanisha mabingwa wa nchi, pia nilikuwa nasomea ukocha kozi mbalimbali, nilirejea nyumbani nikiwa nimepata elimu zaidi," anasimulia.

Anasema kitu kikubwa alichojifunza akiwa Japan wanafundisha maisha halisi mchezaji kujua ataishi vipi baada ya kustafu kazi yake, akitofautisha na hapa nchini.

Mbali na hilo, anakemea ishu ya ushirikina michezoni kwamba inawafanya mafanikio ya wachezaji wengi kugawana na waganga.

"Japokuwa sijawahi kuyashuhudia hayo, ila kwa Afrika yapo sana hayo ndiyo maana wakipata pesa wanagawana na waganga, ifike hatua waanze kumtanguliza Mungu kila mmoja kwa dini yake atafanikiwa," anasema.

Anawaomba wakongwe kwenye mchezo huo, kuungana kwa pamoja kuanza kuinua vipaji vya vijana na kuwasaidia kufurahia matunda ya kazi zao kwa kuwatafutia fursa zinazolipa na wapate stahiki zao.


Ni shabiki wa Simba

Anasema ni shabiki wa Simba kindakindaki, lakini kwa sasa anamkubali mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele kwa namna anavyoonyesha uwezo wa kuisaidia timu yake, jambo analotamani lifanyike ndani ya kikosi cha Simba.

"Sina maana kwamba Simba haina wachezaji wazuri, ila natamani wawe kwenye kiwango cha Mayele, timu inakuwa na uhakika wa kupata mabao, kama ilivyokuwa kwenye miaka minne nyuma, naamini hilo linawezekana," anasema.


Sababu kupigana na Cheka

Anasema kuna wakati alikuwa anacheza mapambano na Francis Cheka kwa sababu ya kuwapa burudani mashabiki, pia alikosa watu wa kushindana nao.

"Nilikuwa nampa moyo Cheka wa kuendelea kupambana, ndiyo maana nilikuwa napanda naye ulingoni, ukiachana na hivyo bondia wa ngumi na mateke anacheza ndondi za kawaida," anasema.

Anasema ili mchezo huo uendelee kuwavutia mashabiki, lazima mabondia wenyewe wajielewe na kubadili mitazamo yao ya kuufanya mchezo huo uwe na heshima na hadhi kubwa.

"Watafute ubingwa wa kweli kweli na si sifa za mitaani, hivyo watakuwa na kazi ya kufanya mazoezi na kujifunza mchezo huo unataka nini, wasichukulie kama filamu za Rambo wajue hii ni kazi kama ilivyo nyingine.

"Pia wasitangulize pesa mbele kabla ya kujenga misingi sahihi ya kuwapa pesa, kizuri kinajiuza wakifanya vizuri watapata mapambano ya kuwalipa, Serikali imeshatia sapoti kwa kuikubali rasmi michezo ya kulipwa, hiyo ni fursa kubwa sana kwao kuanza kuonyesha juhudi zao.

Mbali na hilo, usmati kwenye kazi hiyo ni muhimu ili kuondoa mitazamo mibaya kwenye jamii kuona ni mchezo wa kihuni. Nilijijua ni nembo ya wengi ndiyo maana nilizingatia zaidi usmati, ubondia si uhuni," anasema.