Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kaseja, Makambo uso kwa uso

Muktasari:

  • Kipa kongwe Juma Kaseja anatarajiwa kukutana  uso kwa uso na mshambuliaji nyota wa Yanga, Herieter Makambo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
  • Kaseja anatarajiwa kuiongoza KMC katika mchezo huo akiwa ndiye mchezaji aliyecheza muda mrefu katika mashindano hayo.

Dar es Salaam. Yanga leo inateremka uwanjani kuwania pointi tatu dhidi ya KMC, lakini macho ya mamia ya mashabiki yatatua kwa kipa nguli, Juma Kaseja.

Kati ya wachezaji 22 watakaovuja jasho kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa leo Uwanja wa Taifa, Kaseja ndiye mchezaji mkongwe kuliko wote.

Baada ya kucheza katika klabu tofauti Moro United, Simba, Yanga, Mbeya City na Kagera Sugar, nguli huyo ametua kwa vijana wa Kinondoni, Dar es Salaam.

Kipa huyo ambaye ni miongoni mwa wachezaji wachache katika Ligi Kuu, anakutana na Yanga aliyowahi kuitumikia  kwa vipindi viwili tofauti.

Kaseja anayeonekana bado yuko kwenye kiwango bora, aliwahi kucheza Yanga msimu 2008/2009 na kurejea Simba kabla ya kujiunga tena Yanga mwaka 2013.

Licha ya kuanza kucheza katika mashindano ya Ligi Kuu mwaka 2000 akiitumikia Moro United, anatarajiwa kuwa kikwazo kwa washambuliaji wa Yanga ambao wataongozwa na Herieter Makambo mwenye mabao matatu.

Katika mchezo huo, kipa huyo atakosa kashikashi ya aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo Obrey Chirwa mwenye rekodi nzuri ya kumtungua kipa huyo.

Chirwa huenda akarejea Yanga katika usajili wa dirisha dogo, baada ya mwanzoni mwa msimu kutimkia Klabu ya Daraja la Pili ya Nogoom El Mostakbal ya Misri.

Chirwa amewahi kumfunga Kaseja mara mbili Mei, mwaka jana Yanga ilipoichapa Kagera Sugar mabao 2-1, akifunga bao moja na jingine Simon Msuva anayecheza Diffaa EL Jadida ya Morocco.

Pia Chirwa alimtungua tena Kaseja Oktoba, mwaka jana kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Yanga iliposhinda mabao 2-1.Bao jingine lilifungwa na Ibrahim Ajibu.

Akiwa Mbeya City, Kaseja aliwahi kufungwa na Yanga mabao 2-0 yaliyofungwa na aliyekuwa beki wa timu hiyo Vincent Bossou na Ammis Tambwe.

Kaseja aliyeanza kucheza soka ya ushindani akiwa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys' mwaka 2001 akitoke Sekondari ya Makongo, atakuwa na kazi ngumu ya kuokoa michomo ya akina Ajibu.

KMC itashuka uwanjani ikiwa na wachezaji wazoefu Hassani Kabunda, Abdulhalim Humoud, Yusuph Ndikumana na Emmanuel Mvuyekure. 

Kocha wa KMC Ettiene Ndayiragije ametamba kuvunja mwiko wa Yanga wa kutopoteza mchezo tangu msimu huu ulipoanza.

"Tunaelewa Yanga iko katika kiwango cha ushindi lakini na sisi ni timu ambayo bado tuko kwenye maboresho, tumejipanga kutokana na mpinzani wetu alivyo ili kuhakikisha tunashinda,” alisema Ndayiragije.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema wamejiandaa vizuri kushinda mchezo ili kuendeleza rekodi nzuri kwenye ligi.

"Mpaka sasa hatujapoteza mchezo, tunahitaji kuendeleza rekodi hiyo katika mchezo dhidi ya KMC. Utakuwa mgumu kwa sababu  tunakutana na timu nzuri, "alisema Zahera.