Kaze akiri kuiwaza Simba

Muktasari:

Baada ya Yanga kupumzisha baadhi ya wachezaji muhimu katika kikosi cha kwanza katika mchezo wa leo dhidi ya Biashara United, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Cedric Kaze amekiri kuwa mchezo dhidi ya Simba ni sababu mojawapo ya maamuzi ya leo.

Baada ya Yanga kupumzisha baadhi ya wachezaji muhimu katika kikosi cha kwanza katika mchezo wa leo dhidi ya Biashara United, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Cedric Kaze amekiri kuwa mchezo dhidi ya Simba ni sababu mojawapo ya maamuzi ya leo.

Mbali na kuuwaza mchezo Simba, Kaze amesema nyota hao walipumzishwa baada ya benchi la ufundi kuona kwamba hawako tayari kiufundi, kimwili, kisaikolojia na kiakili kuipa timu matokeo na kutekeleza mipango ya kikosi hicho.

Yanga imebanwa mbavu leo katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na Biashara United kwa kulazimishwa sare ya 1-1.

Ambapo baadhi ya wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza Djigui Diarra, Yanick Bangala, Abubakar Salum (sureboy) walipumzishwa na kuishuhudia mechi wakiwa jukwaani.

Huku Kibwana Shomari nae akiwa hajajumuishwa kwenye kikosi cha leo wakati Khalid Aucho na Saido Ntibazonkiza wakianzia benchi huku Aucho akishindwa kabisa kutumika kwenye mchezo huo.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, Kaze amesema mbali na mambo mengine mchezo wa nusu fainali ya kombe la shirikisho la Azam wa Jumamosi dhidi ya Simba ni sababu sababu mojawapo ya kutowajumuisha mastaa hao.

Kwa upande wao Simba nao walipumzisha baadhi ya wachezaji katika mchezo wa jana dhidi ya Geita Gold akiwemo beki kisiki, Henock Inonga na Aishi Manula.

"Tulicheza ijumaa leo ni Jumatatu mwili wa mchezaji kisayansi unapaswa urudi kwenye hali yake baada ya masaa 72 (siku tatu) sasa wachezaji wengi waliocheza mchezo wa ijumaa tunaamini kuwa leo hawakuwa katika kiwango cha kutupatia kitu ambacho tulikuwa tunatafuta kwenye mechi ya leo.

"Lakini pia hatuwezi kujifichia nyuma ya hicho, na pia mchezo wa Jumamosi wa nusu fainali tunatamani kwenda fainali kwahiyo na hiyo tunaiangalia lakini part kubwa ni recovery," amesema Kaze.