Kiboko ya Argentina, apewa shavu Tunisia
Muktasari:
- Sabri Lamouchi alitimuliwa jana Jumatatu kufuatia kipigo cha mabao 5-1 ambacho Tunisia ilikipata kutoka kwa Sweden, Jumapili.
Siku moja baada ya kumtimua Sabri Lamouchi, Tunisia imemtangaza Mfaransa Herve Renard kuwa Kocha wake Mkuu kwa mechi zote zilizobakia za Kombe la Dunia.
Sabri Lamouchi alitimuliwa jana Jumatatu kufuatia kipigo cha mabao 5-1 ambacho Tunisia ilikipata kutoka kwa Sweden, Jumapili.
Taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tunisia, imeeleza kwamba Renard anaanza majukumu hayo sasa.
“Shirikisho la Mpira wa Miguu Tunisia linatangaza kuteuliwa kwa Herve Renard kuiongoza timu ya taifa hadi mwishoni mwa Kombe la Dunia 2026,” imesema taarifa ya shirikisho hilo.
Herve Renard ni miongoni mwa makocha wenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya kimataifa na soka la Afrika kiujumla.
Kocha mpya wa Tunisia, Herve Renard. Picha na Mtandao
Mwaka 2022, Renard aliishtua dunia baada ya kuiongoza Saudi Arabia kuibuka na ushindi wa bao 2-1 katika mechi dhidi ya Argentina.
Inaelezwa kwamba mara baada ya Kombe la Dunia, Tunisia itampa mkataba wa muda mrefu Renard ambaye amewahi pia kuzinoa timu za taifa za Morocco na Zambia.
Hervé Renard ni raia wa Ufaransa aliyezaliwa katika mji wa Aix-les-Bains, Septemba 30, 1968.
Alicheza soka la kulipwa kwa miaka 15 nchini Ufaransa katika klabu za AS Cannes, Stade de Vallauris na SC Draguignan.
Baada ya kustaafu kucheza soka la kulipwa, alifanya kazi ya usafi katika klabu ya Draguignan kabla ya kuanzisha kampuni yake binafsi ya usafi.
Renard alifundisha klabu kadhaa barani Ulaya na Asia kabla ya kupewa jukumu la kuinoa timu ya taifa ya Zambia.
Aliiongoza Zambia kufika robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 14.
Baadaye aliondoka na kuiongoza timu ya taifa ya Angola, lakini alijiuzulu baada ya miezi saba pekee.
Mwaka 2011, Renard alirejea Zambia na kuiwezesha kutwaa taji lake la kwanza la AFCON mwaka 2012.
Hata hivyo, mwaka uliofuata timu hiyo ilitolewa katika hatua ya makundi, na mwezi Oktoba, 2013 aliachana na Zambia na kujiunga na klabu ya FC Sochaux ya Ufaransa.
Baada ya kipindi kifupi akiwa Sochaux, Renard aliondoka mwezi Aprili, 2014 kufuatia klabu hiyo kushuka daraja, na mwezi Mei mwaka huo akateuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ivory Coast.
Mwaka 2015, Renard aliandika historia kwa kuwa kocha wa kwanza kushinda AFCON akiwa na mataifa mawili tofauti, baada ya kuiongoza Ivory Coast kutwaa ubingwa huo.