Prime
Kibu: Kwa Mpanzu patachimbika
Muktasari:
- Kibu ambaye ni miongoni mwa washambuliaji wanaotegemea na Taifa Stars amezungumzia pia ujio wa winga mpya ambaye Simba imemtambulisha ,Ellie Mpanzu alipoulizwa juu na namna itakavyokuwa mara baada ya dirisha dogo lijalo la Desemba 2024-Januari 2025 kufunguliwa na usajili wa mchezaji huyo mpya Msimbazi kuthibitishwa na mamlaka za soka nchini.
Staa wa Simba, Kibu Denis amefanya mahojiano maalum na Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam na kufafanua mambo kadhaa ikiwemo mwenendo wake pamoja na klabu yake msimu huu.
Kibu ambaye ni miongoni mwa washambuliaji wanaotegemea na Taifa Stars amezungumzia pia ujio wa winga mpya ambaye Simba imemtambulisha ,Ellie Mpanzu alipoulizwa juu na namna itakavyokuwa mara baada ya dirisha dogo lijalo la Desemba 2024-Januari 2025 kufunguliwa na usajili wa mchezaji huyo mpya Msimbazi kuthibitishwa na mamlaka za soka nchini.
Kibu anasema kusajiliwa kwa Mpanzu kunamuongezea morali ya kujituma na kupigania namba katika kikosi cha kwanza.
“Napenda ushindani utafanya niongezee bidii ya mazoezi ili kumshawishi kocha kuendelea kuniamini kunipa nafasi ya kucheza,” anasema mchezaji huyo.
“Hata ningeletewa Cristiano Ronaldo wa Al Nassr, bado ningefurahia kucheza naye, kwani ubora wake ungenifanya kutamani kujifunza vitu vya kunifanya kocha aone umuhimu wangu kikosini.”
Kibu ambaye msimu uliopita alifunga bao moja katika Ligi Kuu Bara, anasema nje na Mpanzu ndani ya kikosi hicho kuna ushindani kila eneo na ni juu ya mchezaji mwenyewe kujituma na kumpa urahisi kocha Davids Fadlu kujua nani amtumie kulingana na mechi husika.
“Mtazamo unaweza ukafanya mchezaji afanye vizuri ama afeli ndio maana nasisitiza napenda ushindani, unanifanya nijitume kwa bidii, kuliko kubweteka na kuona nimemaliza kazi,” alisema Kibu ambaye aliifungia bao moja Simba katika mchezo wa pili wa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikishinda 3-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya.
KUTOKA NGARA
Kibu anasema amepambana sana katika maisha yake ya soka na haikuwa rahisi kufika hapo alipo kwani lengo lilikuwa kuhakikisha kwamba anatimiza ndoto zake,
“Jambo la msingi ni kujituma kwa bidii bila kukata tamaa, nje na hapo itaishia kuwa ndoto isiyogeuka halisi. Haikuwa rahisi hadi jina langu kujulikana nilianzia Ngara huko na sasa nipo Simba,” anasema.
Anasema ukubwa wa jila lake katika soka ulikuja baada ya kujiunga na Simba 2021 akitokea Mbeya City, ukamfanya kuongeza umakini wa kuwaza kufanya makubwa zaidi kila anapopata nafasi ya kucheza.
Tangu ajiunge na timu hiyo anataja baadhi ya mechi ambazo hatazisahau katika maisha yake kuwa ni dhidi ya Raja Casablanca iliyowafunga mabao 6-0 na Al Ahly ya Misri msimu wa 2022/23.
“Ingawa matokeo hayakuwa mazuri upande wetu, lakini ilikuwa ni mechi ya viwango vya juu kwa wachezaji wa timu zote. Hizo ni baadhi ya mechi, (ila) zipo nyingi. Naamini (msimu huu) kadri muda unavyokwenda matunda yataonekana,” anasema Kibu.
ILIKUWAJE HAKUWEPO
Akizungumzia kambi ya Simba msimu huu iliyokuwa Misri ambapo hakuwapo, Kibu anasema kuchelewa kujiunga na timu haikuwa ishu kubwa kivile kama ambavyo ilionekana kujadiliwa sana na watu mitandaoni, kwani alikuwa na ruhusa ya kocha.
“Mimi ni mchezaji. Nafahamu ni namna gani ya kulinda kiwango changu, muda wote nakuwa tayari kwa ajili ya kucheza,” anasema.
Anasema aliwasiliana na kocha Fadlu Davids ambaye alimpa maelekezo ya kitu gani alipaswa kufanya kwa ajili ya kuimarisha kiwango chake, alizingatia na sasa anaendelea na majukumu yake kama kawaida.
Anapoulizwa vipi safari yake ya nje ya nchi aliyodaiwa kwenda Klabu ya Kristiansund BK ya Norway kufanya majaribio,
nyota huyo anajibu,”safari gani, mimi sikuwa na safari yoyote.” Jibu lake fupi liliashiria kwamba hakutaka suala hilo kulizungumzia mbele ya Mwanaspoti.
Mwanaspoti linafahamu Kibu alikwenda kufanya majaribio katika klabu hiyo, lakini dili lake lilikwama kutokana na Simba kuhitaji mkwanja mrefu.
Hata hivyo, anachokiona msimu huu ni kwamba Simba inakwenda kufanya mambo makubwa ikiwemo kuchukua ubingwa katika michuano mbalimbali inayoshiriki.
“Mashabiki watuamini, tushirikiane kufanikisha malengo yetu. Wachezaji wapya waliokuja wana uwezo mkubwa, kikosi ni kipana mfano katika nafasi yangu nisipokuwepo anaweza akacheza Edwin Balua, Saleh Karabaka, Ladack Chasambi na wengine, hivyo wachezaji wao tupo tayari kupambana kwa jasho na damu,” anasema.
ANAKIPIGA BEKI
Mwanaspoti linapomuuliza Kibu ikitokea beki akaumia kama anaweza kuziba pengo? Anajibu: “Nina uwezo wa kucheza kama beki wa kulia. Ndivyo ilivyo kwenye soka la kisasa na winga yoyote anaweza akafanya jukumu hilo, ndio maana unaona naweza kushambulia na kuisaidia timu kukaba.”
Je, unataka kufahamu nani anampa moyo pindi anapokuwa anapitia katika nyakati ngumu, jibu lake ni hili: “Mama na mke wangu wananiambia ninapopitia changamoto yoyote napaswa kumshukuru Mungu na kuchukulia maisha ndivyo yalivyo. Lazima yaendelee kwa namna yoyote ile.”
Fadlu anamzungumzia Kibu? “Ni mchezaji mzuri, napenda anavyoshambulia na kuisaidia timu kukaba, ila wachezaji wote wanahitaji muda ili kuwa sawa. Ndio kwanza ligi imeanza naamini tutafanya vizuri.”