Kiduku: Sikutarajia Mbabe apigwe

Sunday October 10 2021
Dilla pic
By Imani Makongoro

Twaha 'Kiduku' Kassim amefichua namna kipigo alichokutana nacho Abdallah Pazi 'Dullah Mbabe' kilivyomtesa huku akibainisha kwamba hakutarajia bondia huyo namba mbili nchini na mpinzani wake wa jadi kwenye uzani wa super middle apigwe.

Mbabe amechapwa na Alex Kabangu wa DRC usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam, pambano ambalo Kiduku anasema limemuumiza na hakutarajia matokeo hayo kwa Mbabe.

Kiduku alionekana akifuatilia pambano hilo kwenye luninga akiwa mjini Morogoro uku akilazilimika kwenda na muvu ya mchezo na wakati mwingine akinyanyuka kwenye kiti na kujishika kichwa kila Mbabe alipokuwa akishambuliwa.

"Nimeumia, niliona kama mimi vile ndiyo nacheza, kuna wakati nilitamani kupiga hata kelele, lakini ndio mchezo, pambano la Mbabe limeniumiza mno," amesema.

Amesema alilifuatilia pambano hilo mwanzo mwisho na kuna muda alishinda kujizuia na kuhisi kama yuko ulingoni.

Kiduku hata hivyo amefichua kwamba Mbabe amepoteza pambano hilo kwa kutopata muda wa kutosha wa kupumzika baada ya pambano baina yao la Agosti.

Advertisement

"Niliposikia anacheza tena nilustuka, maana pambano letu lilikuwa tafu, hivyo alihitaji muda wa kupumzika kabla ya kurudi ulingoni.

"Mimi tangu pambano lile, kesho Jumatatu ndio naanza mazoezi rasmi, nilipumzika sababu lilikuwa ni gumu, Mbabe yeye aliamua kucheza, naamini hicho pia kimechangia.

"Ila ni bondia mzuri pamoja na kwamba amepoteza pambano hilo, ila anamuda wa kujipanga na kuwa mkali zaidi," anasema.

Anasema kabla ya pambano hilo alimpigia Simu Mbabe na kuzungumza naye mawili matatu na kumtakia kila la heri.

"Nilimposti pia kwenye page yangu ya insta, mimi na Mbabe ni mahasimu ulingoni tu, baada ya raundi kuisha ni marafiki, nimeumizwa mno na matokeo yale kwa sababu napenda sana mafanikio ya mabondia wetu wanapocheza na wageni.

Advertisement