Kinachompeleka Mkude Hospitali

Thursday June 10 2021
mkudepic
By Mwandishi Wetu

JUZI Jumanne Kamati ya Nidhamu ya klabu ya Simba ilishindwa kutoa hukumu ya kiungo Jonas Mkude anayetuhumiwa kwa utovu wa nidhamu ikitaka apelekwe hospitali ya Rufaa ya Taifa, Muhimbili kwa ajili ya vipimo vya afya.

Kamati hiyo ipo chini ya Mwenyekiti Kamanda wa polisi mstaafu, Suleiman Kova aliyewataka viongozi wa Simba kumpeleka mchezaji huyo kwa ajili ya vipimo vya kitabibu vitakavyowapa mwongozo wa namna ya kutoa hukumu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kova alisema mchezaji huyo ana makosa ya kujirudia na kwenye kamati yao hii ni mara ya tatu kupelekwa hivyo kuhisi kuna shida nyingine ya kiafya inayosababisha kufanya mambo kinyume na taratibu za kazi.

Kova alisema matatizo kama ya Mkude ya utovu wa nidhamu huwa yanatokea kwa wachezaji wengi ulimwengu hivyo hushauri kupelekwa hospitali kwa uchunguzi wa afya zao ili kujua namna ya kudili na wachezaji wa namna hiyo. “Makosa yake ni ya kujirudia, sasa haiwezekani mchezaji mmoja huyo huyo akawa anafanya makosa hayo hayo, si kwenye kamati tu hata huko Utawala mara kadhaa anakalishwa chini kuonywa na kuomba msamaha, ni jambo la kushangaza.

“Hivyo tumeona kutoa hukumu pasipo kujua tatizo lake kitabibu haitakuwa sawa, anapaswa kuhukumiwa kulingana na tatizo lake kiafya kama watakavyotuelekeza madaktari.

“Hospitalini huwa wanaangalia mambo mengi yanayosababisha tabia kama hizi, saikolojia, msongo wa mawazo, utumiaji sugu wa vinywaji vikali na mambo mengine, maana huyu ni binadamu, majibu yatakayotoka ndiyo yataelekeza hukumu yake iwe ya namna gani, Mkude ni kijana bado anahitaji kusaidiwa ndio maana adhabu yake itategemea na taarifa ya daktari,” alisema.Kova alisema kwasasa kuweka wazi muda wa hukumu yake sio rahisi hadi pale viongozi na madaktari watakapokubaliana ni lini mchezaji huyo apelekwe hospitali huku akiweka wazi kuchagua hospitali hiyo kwasababu ina madaktari wa aina yote watakaoweza kushughulikia suala hilo.

Advertisement
Advertisement