Kipa Ken Gold amuota Chama
Muktasari:
- Mhagama ambaye anacheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza amekuwa na kiwango bora huku akionekana kuaminiwa kikosini kwa kupewa nafasi chini ya kocha Jumanne Challe.
Licha ya matokeo wanayopitia Ken Gold, lakini kipa wa timu hiyo, Castor Mhagama amesema anaridhishwa na kiwango chake huku akimtaja kiungo wa Yanga, Clatous Chama kumpa wakati mgumu walipokutana majuzi kwenye Uwanja wa Sokoine.
Mhagama ambaye anacheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza amekuwa na kiwango bora huku akionekana kuaminiwa kikosini kwa kupewa nafasi chini ya kocha Jumanne Challe.
Ken Gold haijawa na matokeo mazuri ikicheza dakika 540 bila ushindi ikiambulia pointi moja tu iliyopata dhidi ya Dodoma Jiji huku ikipoteza michezo mitano mfululizo.
Timu hiyo ambayo ni msimu wa kwanza kucheza Ligi Kuu ndio wanaburuza mkia na kuwa miongoni mwa timu tatu ambazo hazijaonja ushindi sawa na Tanzania Prisons na Pamba Jiji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mhagama amesema matokeo hayajawa mazuri akieleza kuwa wanachopitia ni upepo mbaya na kuwa kinachompa matumaini ni ubora alionao.
Amesema katika mechi walizocheza mchezo dhidi ya Yanga alikutana na upinzani mkali kwa straika wa vigogo hao kumsumbua langoni na kwamba Chama hakumpa uhuru.
"Mechi dhidi ya Yanga ilikuwa ngumu nilipambana kadri ya uwezo wangu, lakini washambuliaji wake walinipa wakati mgumu mno haswa Chama ambaye hakunipa uhuru muda wote," amesema Mhagama.
Kipa huyo aliyewahi kupita timu ya vijana (U20) ya Mbeya City ameongeza kuwa wanaamini katika mechi zinazofuata watafanya vizuri kutokana na kila mchezo kujifunza kitu kipya.