Kisa kichapo, Arteta alalamikia mipira

Muktasari:
Fainali ya EFL itakutanisha mshindi wa mechi kati ya Arsenal na Newcastle United na wa mechi kati ya Tottenham Hotspur na Liverpool.
Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta amelalamikia mipira akidai imechangia timu yake ipoteze kwa mabao 2-0 nyumbani mbele ya Newcastle United jana katika nusu fainali ya kwanza ya Kombe la EFL.
Mabao ya Alexander Isak na Anthony Gordon yaliihakikishia Newcastle United ushindi huo ambao unailazimisha Arsenal kupata ushindi mnono ugenini katika mechi ya marudiano, Februari 2 mwaka huu ili itinge fainali ya mashindano hayo.
Baada ya timu yake kupoteza nyumbani, Arteta amedai mipira iliyotumika jana imechangia kuwafanya wapoteze mechi.
“Tumepiga mipira mingi juu ya mtambaa panya na ilikuwa mtego kwamba mipira hii inapaa sana.
“Lakini mwisho wa siku hiyo imeshaenda. Hakuna namna itarudi nyuma. Sasa ni kuhusu mechi zilizo mbele na hiyo ndio dunia yetu na uhalisia wake,” alisema Arteta.
Mipira ambayo imekuwa ikitumika katika mashindano ya EFL inatengenezwa na kampuni ya Puma wakati ile inayotumika kwenye Ligi Kuu England (EPL) ni ya kampuni ya Nike.
Lakini katika hali ya kushangaza, Arsenal imefunga mabao nane (8) katika mechi mbili za EFL ikitumia mipira hiyohiyo ya Puma ambayo Arteta ameilalamikia.