Kisa kichapo vyombo vya habari Hispania vyaiwashia moto Barcelona
Muktasari:
- Gazeti la Sport nalo limeilalamikia Barcelona likiandika: “Si hii, Barca!” likidai timu hiyo haina uhusiano na ile inayocheza vizuri LaLiga.
Vyombo vya habari nchini Hispania vimeichana Barcelona bila huruma baada ya timu hiyo kuonyesha kiwango cha kusikitisha kwenye kipigo cha 3-0 kutoka kwa Chelsea usiku wa jana Jumanne Novemba 25, 2025 kwenye Ligi ya Mabingwa.
Katika mechezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, London, Chelsea ilianza kwa kasi na kufunga bao ndani ya dakika 4 za mwanzo kabla bao hilo kufutwa. Lakini dakika ya 27 ndipo mkasa halisi ulipoikuta Barcelona baada ya beki, Jules Kounde kujifunga bao la kwanza.
Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Ronald Araujo kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kufuatia kumchezea vibaya Marc Cucurella. Kuanzia hapo, kikosi cha Hansi Flick kilionekana kupotea kabisa.
Magazeti ya Hispania yafunguka
Mundo Deportivo limeandika kuwa, “Barcelona ilipotea kabisa” na kuongeza kuwa Chelsea ilipaswa kufunga zaidi kutokana na udhaifu wa Barca.
Gazeti la AS likaita mechi hiyo “Ndoto mbaya”, likisema Barcelona ilikanyagwa na Chelsea na kujiingiza yenyewe kwenye balaa.
Kwa upande wa Catalonia, L’Esportiu liliiita Barcelona “balaa tupu”, likisema timu imeonyesha kiwango duni mno na kuonekana rahisi kufungwa. “Kutolewa kwa Araujo kuligeuza kipindi cha pili kuwa mchezo wa aibu,” ukurasa wake wa mbele uliandika.
Gazeti la Sport nalo limeilalamikia Barcelona likiandika: “Si hii, Barca!” likidai timu hiyo haina uhusiano na ile inayocheza vizuri LaLiga. Wakaongeza kuwa mradi wa Hansi Flick unapaswa kuangaliwa upya kabisa kwa sababu kikosi kilionekana “hakina uimara”.
Ufaulu wa wachezaji
Ndani ya magazeti, mambo yalikuwa mabaya zaidi:
Lamine Yamal alipewa 4/10 tu kwenye mechi yake ya kwanza England. Alizimwa na Cucurella kiasi kwamba alipotolewa akikumbana na matusi ya mzaha kutoka kwa mashabiki wa Chelsea.
Marcus Rashford, aliyeingia kipindi cha pili, naye alipata ripoti mbaya: “Hakusaidia chochote. Hakutokea, wala hakujitolea.”
Lewandowski, Christensen, Eric Garcia, Cubarsi, na Frenkie de Jong pia walipewa alama za chini za kiwango walichokionesha.
Walioumia zaidi ni Araujo na Kounde, ambao wote walipata 3/10.
Mchezaji pekee aliyeonekana kama mtu mwenye uhai ni Alejandro Balde, lakini hata yeye amepewa 6/10 tu.
“Huyu Cucurella mliachaje atoke Barca?”
Gazeti la Marca halikushughulikia sana kichapo. Walichokifanya ni kugeuza mzani tu: wakauliza Barca waliwezaje kumpoteza Marc Cucurella, mzawa wa La Masia, ambaye hakuwahi kuchezeshwa kwenye timu kubwa kabla ya kuuzwa.
Cucurella, aliyeonyesha kiwango cha juu dhidi ya Barca, alipewa ubora wa 9/10 na Daily Mail Sport na kusifiwa na Wayne Rooney kama beki bora wa kushoto kwa muda mrefu.
Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, naye alisema: “Cucu anatusaidia kila mara. Ngazi yake iko juu sana. Tunafurahi sana kuwa naye.”
Barca ilimkataa Estevão
Gazeti Sport pia liliibua swali lingine: kwa nini Barcelona hawakumsajili Estevão aliyefunga bao kali usiku huo?
Inadaiwa kijana huyo alikuwa tayari kujiunga na Barcelona awali, lakini dili likakataliwa kwa sababu nafasi yake ingemgusa Lamine Yamal.