Kitambala alivyokuja na bahati Azam
Mshambuliaji wa Klabu ya Azam, Jephte Kitambala. Picha na Mtandao
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Klabu ya Azam, Jephte Kitambala ni kama alikuja katika wakati sahihi ndani ya kikosi hicho cha matajiri wa Chamazi kinachonolewa na kocha Florent Ibenge ambaye aliwaongoza nyota wake katika safari ya kihistoria ambayo Azam ilikuwa ikiishia njiani kipindi ilipokuwa ikisafiri katika miaka ya nyuma.
Kitambala ambaye ni nyota wa Kimataifa kutokea DR Congo alijiunga na Klabu ya Azam mwanzoni mwa msimu huu wa 2025/2026 akitokea katika Klabu ya AS Maniema Union ya huko kwao DR Congo. Kabla ya kutua Maniema Union, Kitambala aliwahi pia kuitumikia TP Mazembe ambayo nayo inashiriki Ligi Kuu ya DR Congo ‘Ligue 1’.
Straika huyu tangu alipotua Azam Agosti 10, 2025 ni dhahiri kabisa ujio wake ndani ya viunga vya Chamazi ulikuwa kama bahati kutokana na mambo makubwa iliyofanya Azam huku na yeye akiandika rekodi kadhaa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu.
Mshambuliaji wa Klabu ya Azam, Jephte Kitambala. Picha na Mtandao
Nyota huyu aliandika rekodi ndani ya kikosi cha Azam baada ya kuifungia timu hiyo bao la kwanza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, kufuatia ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-1, dhidi ya Nairobi United ya Kenya, Januari 25, 2026.
Ushindi huo kwa Azam ulikuwa wa kwanza katika michuno ya Kombe la Shirikisho msimu huu baada ya kuchapwa mechi mbili mfululizo za hatua ya makundi, iliporuhusu kipigo cha mabao 2-0, dhidi ya Maniema Union ya DR Congo, kisha ilipoteza bao 1-0 kutoka kwa Wydad Casablanca ya Morocco.
Azam FC iliandika historia mpya katika Michuano ya CAF, baada ya timu hiyo kuandika rekodi ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwakwe Julai 23, 2004 ikifahamika kwa jina la Mzizima FC.
Matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam, waliopanda rasmi Ligi Kuu Julai 27, 2008, waliweka historia mpya chini ya Kocha Mkuu, Mkongomani, Florent Ibenge aliyejiunga na timu hiyo Julai 5, 2025, akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan.
Katika Ligi Kuu mambo yanaonekana kumwendea tofauti mshambuliaji huyu kwani katika michezo 14 ambayo tayari amecheza, Kitambala amebahatika kutikisa nyavu za wapinzani mara mbili tu akifanya hivyo katika mechi dhidi ya Simba na Coastal Union huku akitumia dakika 822.
Kabla ya kutua ndani ya kikosi cha Azam, Kitambala alianza kuonyesha makali yake alipokuwa akicheza katika mshindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN 2024) yaliyofanyika kwa pamoja katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Katika mashindano hayo timu ya taifa ya DR Congo ilipangwa kundi A na timu za Kenya ambao walikuwa wenyeji huku timu nyingine zilikuwa ni Morocco ambao ndio walitwaa ubingwa wa michuano hiyo pamoja na Zambia. Katika mechi hizo za makundi mshambuliaji huyu alihusika katika mabao matatu baada ya kupachika mawili na kutoa pasi moja ya mwisho. Na alipotua katika kikosi cha Azam alionekana kuendeleza makali yake licha ya upepo wa mabao kumkatia hivi karibuni.
Hata hivyo, kuanza vibaya kwa mshambuliaji huyo si jambo geni kwa baadhi ya wachezaji wa mpira wa miguu au ndio kumaanisha kwamba ameshindwa kufunga, kwani ni jambo la kawaida kwa mwanasoka yoyote yule hususan washambuliaji ambapo miongoni mwao wamekuwa wakianza polepole lakini baadaye huwa wanakuja kufanya vizuri. Katika mpira wa miguu wakati mwingine mchezaji huwa anahitaji kupata muda wa kutosha ili kuyazoea mazingira ya ligi husika na ndicho kitu anachokipitia Kitambala pale Azam.
Mshambuliaji wa Klabu ya Azam, Jephte Kitambala. Picha na Mtandao
Kitambala ambaye anasifika kuwa na kasi, nguvu na uwezo mkubwa wa kumalizia nafasi alitarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Azam ambapo Klabu hiyo ilijipanga msimu huu kuhakikisha inapambana kushindania taji la Ligi Kuu ambalo haijawahi kurudia kutwaa tena tangu ilipofanya hivyo msimu wa 2013/2014.
Hata hivyo, Azam inaonekana bado ipo kwenye mbio za kutwaa Ubingwa msimu huu kwani hadi sasa Matajiri hao wa Chamazi hawajaruhusu kupoteza mchezo wowote katika mechi za ligi wakishinda mara nane na kutoa sare sita huku wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 34.
Kitambala bado anaendelea kuitumikia Azam FC huku jina lake likisalia daima katika vitabu vya kumbukumbu ndani ya Klabu hiyo kwani ni yeye ndiye aliyeifungia Azam bao la kwanza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika pia akiwa ni miongoni mwa wachezaji walioandika historia ya kuipeleka Azam kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi ya mashindano hayo ya pili kwa ukubwa Afrika katika ngazi ya Vilabu.
Mshambuliaji huyu alisaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Azam FC na mkataba huo utamalizika ifikapo Juni 30, 2026. Kitambala alizaliwa Mei 3, 1999 huko jijini Kinshasa, DR Congo.