Prime
Simba yamuweka mtegoni Ibenge Azam
Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Azam inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na pointi 33 ilizokusanya katika michezo 17.
Dar es Salaam. Sare ya bila kufungana dhidi ya Simba juzi katika Uwanja wa Azam Complex imeifanya Azam FC chini ya Kocha Florent Ibenge kujihakikishia ubabe dhidi ya Simba msimu huu.
Hata ikitokea timu hizo zikakutana katika Kombe la Shirikisho la CRDB na Simba ikapata ushindi, bado Azam FC itabakia kuwa mtemi wake kwa vile hadi sasa timu hizo zimekutana mara tatu ambapo mara mbili ni katika Ligi Kuu ya NBC na mara moja katika Kombe la Mapinduzi na kati ya hizo, Azam FC imepata ushindi mara mbili na zimetoka sare moja huku Simba ikiwa haijafunga bao lolote na yenyewe imefungwa mabao matatu.
Pamoja na sare hiyo kulinda utemi wa Ibenge dhidi ya Simba, kwa upande mwingine imemuweka Kocha huyo katika uwezekano wa kuvunja rekodi isiyovutia ambayo timu hiyo inayo katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Rekodi hiyo ambayo inamnyemelea Ibenge msimu huu ni ya Azam FC kupata idadi kubwa zaidi ya matokeo ya sare kwa msimu ambayo hadi sasa inashikiliwa na msimu wa 2018/2019.
Katika msimu wa 2018/2019, Azam FC ilipata matokeo ya sare katika michezo 12 ya Ligi Kuu ambayo ni idadi kubwa zaidi ya michezo ambayo timu hiyo imepata sare kwa msimu tangu ilipoanza kushiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu wa 2008/2009.
Azam FC katika msimu huu, imeshatoka sare katika mechi tisa ambapo ikipata matokeo ya namna hiyo katika michezo mitatu kati ya 13 iliyobakiza, itafikia rekodi ya msimu wa 2018/2019 na ikiwa itatoka sare katika mechi nne maana yake itavunja rekodi hiyo ya sare nyingi.
Katika msimu huu mechi tisa ambazo Azam FC imetoka sare ni dhidi ya Simba, Mashujaa FC, Yanga, Tanzania Prisons, Pamba Jiji, Fountain Gate, Singida Black Stars, Namungo FC na JKT Tanzania.
Timu hiyo katika michezo tisa ambayo imetoka sare, michezo mitatu ndio ilikuwa na sare ya mabao ambayo ni dhidi ya Namungo, JKT Tanzania na Pamba Jiji FC na mechi zilizobakia sita hazikuwa na mabao.