Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kiungo Senegal ajiweka kando akitoa sharti moja

Muktasari:

  • Pape Gueye amecheza mechi za Senegal katika Kombe la Dunia 2026, akifunga mabao mawili na kupiga pasi moja ya mwisho.

Saa chache baada ya Senegal kutupwa nje kwenye Fainali za Kombe la Dunia baada ya kufungwa mabao 3-2 na Ubelgiji, kiungo Pape Gueye ametangaza kujiweka kando kuichezea timu hiyo.

Gueye anayechezea Villarreal ya Hispania, amesema kwamba hatoichezea Senegal kama benchi la ufundi la sasa litaendelea kuwa chini ya kocha Pape Thiaw.

"Nitapumzika kuchezea timu ya taifa kwa muda wote ambao benchi hili la ufundi litaendelea kuisimamia timu,” amesema Gueye.

Gueye ameshindwa kuanika hadharani nini hasa kimetokea baina yake na benchi hilo la ufundi la Senegal hadi akachukua uamuzi huo.

Kiungo huyo hata hivyo amesema kwamba anajiandaa kujulisha umma sababu zilizoikwamisha Senegal katika mashindano hayo siku kadhaa zijazo.

“Nitakuja baadaye kuzungumzia sababu za kutolewa mashindanoni. Lakini leo natangaza kwamba kwa vile benchi hili la ufundi linaendelea kuwepo, nitasimama kuichezea timu ya taifa ya Senegal,” amesema Gueye.

Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, Gueye amecheza mechi nne, akifunga mabao mawili na kupiga pasi moja ya mwisho.

Senegal imeondolewa kwa namna ya kushangaza na Ubelgiji katika mechi ya hatua ya 32 bora iliyochezwa alfajiri ya kuamkia leo, Alhamisi, Julai 2, 2026 kwa muda wa Afrika Mashariki.

Iliongoza kwa mabao 2-0 hadi katika dakika ya 84 ya mechi lakini Ubelgiji ilifunga mabao mawili katika dakika tano za mwisho na kufanya mechi hiyo iende katika dakika 30 za nyongeza.

Wakati wengi wakiamini kwamba mechi hiyo ingemalizika kwa mikwaju ya penalti, Ubelgiji ilifunga bao la tatu katika dakika ya 120 na hivyo kuzika rasmi ndoto ya Senegal kusonga mbele.