Kocha atamba Nigeria haijatoka kinyonge
Dar es Salaam. Kocha mkuu wa Nigeria, Eric Chelle ametamba kuwa timu yake imemaliza kikubwa fainali za CHAN na pamoja na kutolewa mapema katika fainali za CHAN 2024.
Licha ya kupata ushindi katika mechi ya mwisho dhidi ya Congo na kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi D, Nigeria imeshindwa kutinga robo fainali huku ikiziacha Sudan na Senegal zikisonga mbele.
Chelle amesema kuwa kufanya vibaya katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Senegal na Sudan kumechangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya waage mashindani lakini wanaamini CHAN imewajenga vyema.
"Najisikia vibaya kwa sababu mechi hii ilikuwa nzuri lakini mechi za mwanzo tulikuwa na makosa.Siamini kama wachezaji wangu wameniangusha. Presha ilikuwa kubwa kwa hawa wachezaji na wakati wanacheza kwa woga.
"Lakini katika mechi ya mwisho dhidi ya Congo, walicheza kwa heshima na ndio maana wamecheza vizuri. Hatukuwa tayari kushiriki haya mashindano," amesema Chelle.
Hata hivyo Nigeria inaondoka katika mashindano hayo ikiwa na uhakika wa kuvuna kiasi cha Dola 300,000 (Sh754 milioni).
Katika robo fainali, Tanzania itacheza na Morocco, Uganda dhidi ya Senegal, Kenya dhidi ya Madagascar na Sudan na Algeria.