Kocha Chelsea apigwa rungu England
Muktasari:
- Kocha huyo raia wa Italia aliondolewa katika benchi baada ya kuvunja sheria na kwenda kushangilia asikoruhusiwa baada ya timu yake kupata bao la ushindi dakika za mwisho za mechi hiyo.
London, England. Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, amefungiwa kwa mchezo mmoja kuiongoza timu yake uwanjani na kutozwa faini ya Pauni 8,000 (zaidi ya Sh25 milioni) na Shirikisho la Soka la England kutoka na kosa alilofanya katika mechi kati ya timu yake na Liverpool.
Kocha huyo raia wa Italia aliondolewa katika benchi baada ya kuvunja sheria na kwenda kushangilia asikoruhusiwa baada ya timu yake kupata bao la ushindi dakika za mwisho za mechi hiyo.
Maresca alikimbia pembeni mwa uwanja kushangilia pamoja na wachezaji wake katika dimba la Stamford Bridge, jambo lililosababisha kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na katika taarifa ya FA ilisema kocha huyo amedhibiwa kwa kuonyesha tabia zisizofaa.
“Enzo Maresca amefungiwa mechi moja na kutozwa faini ya Pauni 8,000 kutokana na kosa alilofanya katika mechi ya Ligi Kuu kati ya Chelsea na Liverpool iliyochezwa Jumamosi, Oktoba 04. Kocha huyo alitumia maneno na tabia zisizofaa wakati wa mchezo, jambo lililosababisha kutolewa katika dk96.
Maresca amekubali kosa hilo na amekubali adhabu yake.”
Katika mchezo huo, Moises Caicedo aliwapatia Chelsea bao la kuongoza kwa shuti kali kipindi cha kwanza kabla ya Cody Gakpo kuisawazishia Liverpool, kisha staa chipukizi Estevao kufunga bao la ushindi katika dakika za ‘jiooni’.
Baada ya mchezo, Maresca alisema kuwa kutolewa kwake “kulistahili kabisa” lakini alifanya vile kutokana na furaha aliyokuwa nayo.
Ushindi huo uliipandisha Chelsea hadi nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa imeshinda mechi tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
Maresca aliiwezesha Chelsea kumaliza nafasi ya nne msimu uliopita, kisha akaiongoza kutwaa taji la UEFA Conference League dhidi ya Real Betis.
Katika majira haya ya kiangazi, kocha huyu pia aliiongoza Chelsea kushinda Kombe la Dunia la Klabu, Marekani.
Chelsea imesafiri kwenda kuivaa Nottingham Forest ugenini katika mechi itakayopigwa Jumamosi ya wikiendi hii kuanzia saa 8:30 mchana.