Kocha: Mtaipenda tu Azam

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Abdihamid Moallin amesema amefurahishwa na ubora wa wachezaji wake wapya ndani ya timu huku akitamba kufanya makubwa msimu 2022/23.

Azam FC ambayo ilitua nchini juzi baada ya kukaa kambini wiki mbili nchini Misri inatarajiwa kucheza mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kutambulisha mastaa wapya kwenye mchezo dhidi ya Zesco utakaochezwa Agosti 14, Uwanja wa Azam Complex.

Akizungumza na Mwanaspoti, Moallin alisema alikuwa na wiki mbili bora Misri na ameona ubora wa kila mchezaji huku akithibitisha kuwa wachezaji wageni wameweza kufiti mfumo wake haraka, hivyo kilichobaki ni ushindani.

“Kwa asilimia kubwa maingizo mapya yameongeza ubora ndani ya timu, kila mchezaji ana kitu cha tofauti, wamefanya vizuri kwenye maandalizi tuliyoyafanya,” alisema.

Akizungumzia mechi ya kirafiki alisema watakuwa na mchezo mmoja kabla ya kuikabili Zesco.

Wakati kocha huyo akishindwa kuweka wazi ni timu gani watacheza nayo, Mwanaspoti limepenyezewa kuwa ni Coastal Union.


MGUNDA AFUNGUKA

Wakati Azam wakificha mechi ya kirafiki dhidi ya Coastal Union, kocha wa timu hiyo, Juma Mgunda alisema watacheza na Azam baada ya mechi ya kirafiki ya kwanza na Namungo FC.

Mgunda alisema: “Tumesajili kikosi kizuri na kuongeza nguvu kila eneo. Tuna matarajio makubwa msimu ujao ili kujiweka fiti baada ya mazoezi ya muda mrefu tumeamua kucheza michezo mitatu miwili Dar es Salaam na mmoja Uwanja wa nyumbani,”

Coastal Union imewauza Victor Akpan (Simba) na Abdul Suleiman ‘Sopu’ (Azam FC imesajili wa wachezaji tisa. Waliosajiliwa ni Optatus Lupekenya (KMKM), Maabad Maulidi (KVZ), Olatoundji Djibril (ASVO Benin), Mahamoud Mroivili (Coin Nord Mitsamiouli), Khatib Kombo (Kipanga), Mukanisa Pembele (Simba Kamikaze Kolwezi), Firdaus Seif Amour (Taifa Jang’ombe),Bertrand Ngafei Konfor (Gor Mahia) na Nimubona Emery (Kayanza United FC)