Kocha Scotland akata tamaa kuingia 32 bora
Muktasari:
- Brazil imemaliza hatua ya makundi ikiwa kinara wa kundi C na poibti saba sawa na Morocco iliyo nafasi ya pili huku Scotland ikishika nafasi ya tatu na pointi zake tatu na inayoshika mkia ni Haiti ambayo haina pointi.
Kocha wa Scotland, Steve Clarke anaamini kwamba timu yake haitoweza kufuzu hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia licha ya kumaliza ikiwa nafasi ya tatu kwenye kundi C ikikusanya pointi tatu.
Kuna uwezekano wa Scotland kuingia hatua ya 32 kupitia nafasi mojawapo kati ya nane zinazoenda kwa timu zilizomaliza katika nafasi ya tatu kwenye makundi huku zikiwa na matokeo bora (best losers).
Kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Brazil alfajiri ya kuamkia leo, Alhamisi, Juni 25, 2026, kimeifanya Scotland kukosa nafasi ya moja kwa moja ya kutinga hatua ya 32 bora na Clarke anadhani kuwa shughuli yao imeishia hapo.
“Ni matokeo tuliyostahili. Unapoipa timu kama Brazil nafasi tulizoipa sisi, tegemea utaadhibiwa. Na hicho ndicho kilichotokea. Nadhani tunarudi nyumbani.
Clarke amesema kuwa pamoja na timu yake kufahamu namna Brazil ilivyo hatari katika eneo la kushambulia. wachezaji wa Scotland wamefanya makosa ambayo yametumiwa vyema na wapinzani wao kupata ushindi.
Hata hivyo amesema kwamba hawezi kutoa lawama kwa wachezaji wake ambao wameiwezesha timu hiyo kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu walipofanya hivyo mwaka 1998.
Amesema ushiriki wao katika mashindano hayo mwaka huu ni darasa la kujipanga kwa ajili ya awamu zijazo.
“Nadhani ukiangalia miili, nguvu na ufundi wa wachezaji wa Brazil na Morocco, unaweza kuona nini tunachotakiwa kukifanya.
“Tunatakiwa kujaribu na kuwa bora katika kuandaa vijana wadogo ambao watamudu kutubeba katika ngazi ya kimataifa,” amesema Clarke.