Kombe la Dunia na historia ya kuibwa

Muktasari:

  • Siku zinazidi kukatika kabla ya kuanza kwa michuano mikubwa zaidi duniani ya mchezo wa soka duniani, kombe la dunia kuanza kule Qatar.

London, England. Siku zinazidi kukatika kabla ya kuanza kwa michuano mikubwa zaidi duniani ya mchezo wa soka duniani, kombe la dunia kuanza kule Qatar.

Moja ya alama kubwa ya michuano hii ni lile kombe ambalo timi hupewa baada ya kuwa bingwa.

Lakini kombe hili lina historia ya kufurahisha kidogo kuanzia la kwanza hadi hili tunalotumia sasa.

kombe lililokuwa linatumika kwa mara ya kwanza liliitwa Victory lakini lilibadilishwa jina na kuitwa Jules Rimet ikiwa ni ishara ya kumuenzi mzee Jules Rimet aliyewahi kuhudumu kama rais wa FIFA na ndio aliyeanzisha michuano hii.

Taji hili lilitumika kuanzia 1930 hadi 1970, baada ya timu ya taifa ya Brazil kulichukua mara tatu na FIFA kuamua kuwapa mazima, hata hivyo likiwa nchini humo Brazil liliibiwa 1983 na hadi leo halijapatikana. Baada ya kombe hilo kupewa Wabrazil, mwaka huo huo FIFA ilitengeneza kombe lingine kupitia Silvia Gazzaniga ambalo ndiyo linatumika hadi leo.

Stori kubwa ipo kwenye kombe la mara ya kwanza lililotumika kuanzia 1930 hadi 1970, wezi walijaribu kuliiba mara mbili na kufanikiwa kulipata katika jaribio la pili.

Mara ya kwanza lilipoibiwa lilivumbuliwa na mbwa ambaye hadi leo amebakia kwenye historia ya vitabu vya soka duniani. Hii hapa stori kamili jinsi lilivyopotea na kupatikana kwa msaada wa mbwa huyo kabla ya kupotea tena.


Ilikuaje

1966, mashindano ya Kombe la Dunia yalikuwa yakifanyika nchini England, January mwaka huo tayari taji lilishawasili nchini humo kusubiria michuano hiyo iliyoanza Julai 11 hadi 30.

Lakini machi 20, walinzi waliokuwa zamu kulinda eneo ambalo kombe hilo lilihifadhiwa waligundua kwamba kombe hilo limeibwa, msako wa kulitafuta ukaanza.

Ilipofika machi 27, jamaa mmoja aliyeitwa David Corbett akiwa na mbwa wake njiani aliyeitwa Pickles walifanikiwa kuliokota taji hilo.

Ilikuwa ni baada ya mbwa huyo kunusa harufu na kuanza kuifuata hadi alipofika kwenye kitu kilichofungwa kwa gazeti kuu kuu mbepezoni ya gari lililoegeshwa na Corbett alipofungua akakutana na kombe lililokuwalimeibiwa.

Hakutaka mambo mengi zaidi ya kuliwasilisha kituo cha polisi na baadae likaenda kukabidhiwa kwa chama cha soka nchini England.

Corbett aliitwa kituoni pia kwa mahojiano zaidi kwa kuwa alikuwa akidhaniwa kwamba huenda alihusika kwenye wizi, lakini baada ya mahojiano hakufunguliwa mashtaka yoyote.

Mwaka huo England ilichukua ubingwa wa kombe hilo na Corbett sambamba na mbwa wake walialikwa kwenye

chakula cha jioni cha kusheherekea ubingwa na wachezaji wa England.

Pia alizawadiwa kiasi cha Pauni 5,000 ambayo kwa sasa inaweza kufikia Pauni 99,000 ikiwa kama sehemu ya zawadi ya kulipata taji hilo, pesa hiyo aliitumia kununua nyumba huko maeno ya Lingfield, Surrey.

Mbwa mwenyewe

Jina lake ni Pickles alizaliwa kati ya 1962 na1963, wakati anafanya tukio hilo la kishujaa anakadiriwa kuwa alikuwa na umri wa miaka minne.

Baada ya tukio hilo mbwa huyu alionekana kwenye filamu ya The Spy with a Cold Nose, ambayo aliigiza na waigizaji maarufu wa wakati huo nchini England, Eric Sykes na June Whitfield.

Alionekana kwenye vipindi mbalimbali vya luninga, pia alitunukiwa tuzo ya mbwa bora wa mwaka, kisha akapewa medali ya fedha ya National Canine Defence League.

Kifo chake pia kilikuwa cha maajabu kama yaliyokuwa maisha yake, tofauti na mbwa wengi ambao huwa wanaugua na kufariki, Pickles kwake haikuwa hivyo.

Ikiwa ni mwaka mmoja tangu aibuke shujaa, 1967 aliaga dunia baada ya kamba yake ya shingoni aliyokuwa amevaa kunasa kwenye tawi la mti na kumkaba shingoni hadi kupoteza maisha.

Chanzo cha kamba hiyo kunasa kwenye tawi ilikuwa ni wakati anajaribu kumkimbiza paka aliyekuwa anapita karibu na nyumbani kwao.

Pickles alizikwa nyuma ya nyumba yao na kola yale ya shingoni ilichukuliwa na kupelekwa kwenye jumba la makumbusho la mpira wa miguu lililopo Jijini Manchester.