Kotei: Simba inatoboa freshi tu!

Monday May 03 2021
YOYOTE PIC 1
By Thobias Sebastian

BAADA ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuipanga Simba na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwenye mechi za robo fainali, nyota wa zamani wa Msimbazi, James Kotei aliyewahi kukipiga Kaizer amesema kwa kinywa kipana ‘Simba inatoboa’ kama alivyosema Patrick Aussems.

Aussems, kocha wa zamani wa Simba na Kotei aliyewahi kukipiga Simba na Kaizer waliliambia Mwanaspoti kwa muda tofauti kwamba kwa namna Simba ilivyoimarika ina nafasi nzuri kutoboa.

Kotei anayekipiga kwa sasa FC Slavija Mazyr iliyopo Ligi Kuu ya Belarusi alisema Simba imeimarika zaidi kuliko kipindi akiichezea aua ilivyo kwa Kaizer, akidai kuanzia wachezaji hadi benchi la ufundi lipo kibingwa zaidi na kwamba wakijipanga watapta matokeo mazuri nje ndani.

“Ukiiangalia Kaizer sio kama niliyokuwa naichezea kwa sasa sio tishio, lakini ina nyota kama kina Khama Billiat, Teddy Akumu, Bernard Parker wanaoweza kuisumbua Simba, ila bado Simba ni bora zaidi kulinganisha na Wasauzi hao,” alisema Kotei.

Mghana huyo alisema japo Simba ni bora, lakini lazima wajue mapema kwamba baada ya ratiba hiyo kutoka hata Kaizer watakuwa wanajindaa zaidi baada ya kujua wanakwenda kucheza na Simba hivyo lazima WEkundu wa Msimbazi wajipange ili kufuzu nuau fainali.

Naye Aussems alisema timu hiyo imeimarika zaidi wakati huu kuwepo na wachezaji wengi bora katika maeneo tofauti.

Advertisement

Aussems anayeifundisha AFC Leopards iliyopo Ligi Kuu ya Kenya, alisema wachezaji waliyopo wakati huu Simba wana uwezo mkubwa wa kuifunika Kaizer na kupata matokeo nyumbani na ugenini, lakini wasijiaminishe moja kwa moja.

“Nilikueleza mapema kabla ya Simba kufika hatua hii kuwa ilivyoimarika wakati huu sioni kama itashindwa kufanya vizuri na ndilo lililotokea na wakikomaa hapo wanavuka kwenda nusu fainali. Kaizer ni timu nzuri yenye uzoefu pia wa michuano ya CAF lakini mechi mbili dhidi ya Simba watakuwa na wakati mgumu,” alisema Aussems na kuongeza;

“Kama kina Clatous Chama, Luis Miquissone, Aishi Manula watakuwa katika viwango bora Simba wanaweza kupoteza kwa idadi ndogo ya mabao ugenini kisha wakaenda Dar es Salaam kupata ushindi mkubwa na wakafuzu robo fainali.”

Aussems, ndiye aliyeipeleka Simba robo fainali ya michuano hiyo ya Afrika msimu wa 2018-2019 na kutolewa na TP Mazembe.

Advertisement