Kutochanja kwamzuia rais kuona mechi ya soka

Muktasari:

Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro amesema jana (Jumapili) kuwa masharti ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Uviko-19, yamesababisha ashindwe kwenda uwanjani kuangalia mechi ya mpira wa miguu, vyombo vya habari vimeripoti.

Sao Paulo, Brazil. Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro amesema jana (Jumapili) kuwa masharti ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Uviko-19, yamesababisha ashindwe kwenda uwanjani kuangalia mechi ya mpira wa miguu, vyombo vya habari vimeripoti.

Rais Bolsonaro alisema alitaka kuangalia mechi ya ubingwa wa soka wa Brazil katika jiji la Santos kati ya wenyeji Santos na Gremio, lakini hakuweza kwa sababu hajapata chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

"Kwa nini kuwe na hati ya chanjo? Nilitaka kuiangalia Santos sasa na wakasema natakiwa nipate chanjo. Kwa nini iwe hivyo?" Bolsonaro amekaririwa na tovuti ya firstpost.com akiwaambia waandishi wa habari.

Bolsonaro, ambaye amekataa kuchanjwa na anahamasisha wengine wafuate msimamo huo, anadai kuwa tayari ana kinga ya mwili kwa sababu alishaambukizwa Covid-19, kwa mujibu wa globeandmail.com.

Haikueleweka kama Bolsonaro, ambaye ni shabiki kindakindaki wa soka na ambaye alitumia wikiendi iliyopita karibu na jiji la Santos, alijaribu kwenda uwanjani au malalamiko yake ni ya kiujumla dhidi ya haja ya kuwa na hati ya ya chanjo ya Covid-19.

Lakini klabu ya Santos ilisema Rais Bolsonaro hakuomba kuhudhuria mechi hiyo ambayo iliisha kwa Santos kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gremio kwenye uwanja wa Vila Belmiro.

HUo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Santos kuruhusu mashabiki tangu kuanza kwa janga la Covid-19, lakini klabu hiyo ilisisitiza kuwa itaruhusu watu waliopata chanjo tu kuingia uwanjani au wale ambao vipimo vitaonyesha hawana maambukizi.

Wiki hii mamlaka ziliruhusu klabu kuingiza asilimia 30 ya uwezo wa uwanja katika mechi za ubingwa wa Brazil.

Masharti yaliyokubaliwa na Shirikisho la Soka la Brazil yanasema watu wote wanaokuwa ndani ya uwanja lazima wawe wamepata chanjo na wamepimwa siku za karibuni.

Kwa sasa Rais Bolsonaro anachunguzwa na seneti ya Brazil kutokana na jinsi alivyoshughulikia janga hilo lililoua maelfu ya watu duniani. Brazil imeshavuka idadi ya watu 600,000 walio na maambukizi, kwa mujibu wa taarifa za wizara ya afya.